Tanzania, Wataalam wa “Visit Finland” wabadilishana uzoefu Kutangaza Utalii

0

Na Mwandishi Wetu, Helsinki

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amekutana na kubadilishana uzoefu wa mikakati ya kutangaza utalii na wataalamu mbalimbali wa utalii wa nchi ya Ufini (Finland).

Katika ziara yake inayoendelea nchini Ufini, Dkt. Abbasi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kuitangaza Tanzania, alianza kwa kukutana na Mjumbe wa “Team Finland” Kamati ya Kitaifa ya Sekta mbalimbali ya kuibrand nchi hiyo, Balozi Paula Parviainen ambaye alieleza jinsi nchi hiyo inavyounganisha sekta mbalimbali katika jukumu moja la kitaifa la kuipa taswira njema nchi hiyo.

Baadaye alikutana na timu ya wataalamu wa “Business Finland” wanaosimamia pia Kikosi cha Kutangaza Utalii wa nchi hiyo kimataifa yaani “Visit Finland” wakiongozwa na Mkurugenzi Mwandamizi wa Masoko ya Kimataifa, Heli Jimenez ambaye alitoa uzoefu wa namna Finland inavyotumia mandhari zake za misitu kuibua zao jipya la utalii uitwao “wellness.” huku Tanzania nayo ikitoa uzoefu wake hasa katika utalii wa safari za kuona wanyama.

Aidha, Katibu Mkuu na ujumbe wake amepata wasaa wa kubadilishana uzoefu na mikakati na Timu ya wataalamu kutoka “Business Helsinki” wanaosimamia pia kampeni ya kiutalii ya jiji la Helsinki ya “Visit Helsinki” na kubadilishana uzoefu namna miji inavyoweza kutumia vivutio vyake kujitangaza kwa ajili ya utalii wa ndani na ule wa kimataifa.

Akitoa uzoefu wake, Meneja Mwandamizi wa Taarifa za Watalii na Ubunifu wa Maudhui, Mari Somero, alisema jiji la Helsinki pekee hupata hadi watalii Milioni 4 kwa mwaka na wameunda timu inayohakikisha kila sekta inatimiza wajibu wake katika kuufanya mji huo kuwa kivutio zaidi.

“Kila tulipokutana na wataalamu wenzetu hawa waliobobea zaidi katika kutangaza utalii mambo mawili yamejitokeza; mosi, wametumia sana mazingira yao kuibua mazao mchanganyiko ya utalii kama vile utalii wa misituni, wakati wa kiangazi na baridi na hata utalii wa mijini (urban tourism).

“Pili, wamewekeza bajeti kubwa kujitangaza kimataifa mpaka wana vituo maalum vyenye maafisa kamili wa utalii katika miji mikubwa ya Ulaya, Asia na Marekani na wametupa uzoefu pia jinsi walivyoshirikiana na kampuni kubwa inayosafirisha zaidi ya watalii milioni 400 kwenda sehemu mbalimbali ya Expedia ya Marekani,” alisema Dkt. Abbasi.

Finland ambayo, tofauti na Tanzania, bado haijarejea kwenye idadi yake ya kawaida ya watalii ikilinganishwa na kabla ya Uviko, kwa takwimu mwaka mmoja uliopita ina jumla ya watalii wa ndani na nje wapatao Milioni 11 huku ikiwa na mapato ya Euro Bilioni 3.4.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here