Tanzania mbioni kutoka kwenye umaskini

0

TANZANIA imeorodheshwa na Kamati ya Sera za Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, kuwa miongoni mwa nchi zinazotazamiwa kufuzu kutoka katika kundi la nchi masikini (Least Developed Countries) kwenda nchi inayoendelea.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakati wa Mkutano wa Awali wa tathmini ya nchi kutoka nchi maskini kwenda nchi inayoendelea inayofanywa na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika lake la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD).

Dkt. Mwamba alisema hatua hiyo imetokana na Tanzania kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miongo miwili iliyopita kupitia uthabiti wa Sera za uchumi zilizosababisha kukua kwa uchumi kwa wastani wa asilimia 6.2 kati ya mwaka 2000 na 2024.

“Pato la mtu kwa mwaka limeongezeka kutoka dola za Marekani 453 mwaka 2000 hadi dola 1,277 kwa mwaka 2023, kiwango cha umasikini uliokithiri kimepungua kutoka asilimia 36 mwaka 2000 hadi asilimia 26 mwaka 2024 kutokana na utekelezaji makini wa sera za fedha na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi”, alisema Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba alisema kuwa Mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa na kubaki kwenye tarakimu moja hali iliyoimarisha uthabiti wa uchumi na kuongeza uwezo wa wananchi kukabiliana na gharama za maisha.

Alisema kuwa kumekuwa na uwekezaji wa kimkakati hususani katika miundombinu ya nishati kupitia utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere Hydropower ambao ni mradi mkubwa wa kitaifa wa ujenzi na uzalishaji wa umeme.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here