Tanzania kuvuna Trilioni 2.3 mradi wa EACOP

0

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ni wa kielelezo na kimkakati kutokana na faida zake mbalimbali ikiwemo kuongeza mapato ya nchi katika kipindi cha ujenzi na uendeshaji kwa kiasi cha Shilingi Trilioni 2.3.

Mbali na hayo, alisema utatoa ajira kwa watanzania, ambapo mpaka sasa umeajiri takriban wananchi 7,584 huku ajira hizo zikitarajiwa kuongezeka.

Matagio alisema hayo wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kukagua utekelezaji wa katika kituo kitakachotumika kupokea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda, ambapo alisema kampuni 146 za kitanzania zimehusika kutoa huduma mbalimbali kwenye mradi na kunufaika kwa takriban Dola za Kimarekani Milioni 246.

Pia, mradi huo umechangia kufanyika kwa manunuzi ya Dola za Marekani Milioni 462 pamoja na vijana wa kitanzania kupata mafunzo ya teknolojia mbalimbali, ambapo ujuzi huo watautumia kwenye miradi mingine ya ujenzi wa mabomba kuelekea nchini Kenya na Zambia.

Alitaja wanahisa wa mradi huo kuwa ni Kampuni ya Total Energies ya Ufaransa (62%), CNOOC ya China (8%), Kampuni ya Mafuta ya Uganda (15%) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (15%).

Alisema, kwa ujumla mradi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 39.2 huku baadhi ya kazi zikikamilika kwa asilimia 100, huku ujenzi wa kiwanda cha kuwekea mabomba mfumo wa kuhifadhi joto cha Sojo ukifikia asilimia 90 na katika eneo la Chongoleani mradi umefikia asilimia takriban 40 na kueleza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2026.

Alieleza kuwa, Serikali inashirikiana vizuri na wanahisa wengine kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na Serikali ya Tanzania imekamilisha kuchangia mtaji wake kama mwanahisa ambapo mpaka leo Serikali.imechangia Dola za Marekani milioni 308 ambayo ni sawa na asilimia 100 ya kiwango ambacho ni cha awali cha gharama za ujenzi kwa asilimia 15 ya hisa za Tanzania.

Kuhusu utwaaji wa ardhi ya mkuza wa EACOP kwa upande wa Tanzania alisema, imekamilika kwa asilimia 99.2 na asilimia iliyobaki inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo masuala ya mirathi. Amesema kuwa kwa upande wa Uganda mradi huo pia unaendelea vizuri.

Mara baada ya kukagua kituo hicho kilichopo Kata ya Chongoleani wilayani Tanga, Mkoa wa Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza alisema Kamati hiyo ambayo inasimamia mipango na uchumi wa nchi imeona mradi wa EACOP una umuhimu kiuchumi hivyo wataendelea kuupa msukumo mkubwa ili ukamilike kwa wakati.

Kamati hiyo imempongeza, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mabadiliko ya kiuchumi anayoyafanya kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama wa EACOP ambayo inaendana na jinsi dunia inavyokwenda kwa sasa.

“Mradi mkubwa kama wa EACOP haukutegemewa kufanyika kwenye nchi za kiafrika lakini maono ya Viongozi Wakuu wa nchi Uganda na Tanzania yamepelekea mradi huu kufanyika ili kuwezesha mafuta sasa kusafirishwa kwa njia ya mabomba ambayo pia yanasaidia katika ulinzi wa mazingira.” alisema Njeza.

Aidha, Kamati hiyo ya Bajeti imeitaka Wizara ya Nishati kuweka kipaumbele katika ujenzi wa mabomba  yakayosafirisha nishati za aina mbalimbali kama vile Gesi na Mafuta na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kituo cha usafirishaji wa nishati hizo barani Afrika.

Vilevile, Kamati imeliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza nguvu ya kuutangaza mradi huo ili wananchi wafahamu jinsi Serikali inavyoendelea kutekeleza miradi yake. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian alisema, mradi wa EACOP una faida mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo kutoa ajira takriban 900, kuongeza mzunguko wa fedha, kuongeza fursa za biashara ikiwemo katika kituo cha kupokelea, kuhifadhi na kusafirikisha mafuta kilichopo Chongoleani Tanga, kuuza rasilimali kama vile simenti na  kupata mapato mbalimbali kupitia ushuru.

Ametilia mkazo masuala ya afya na usalama pahala pa kazi katika miradi mbalimbali nchini ambapo ameipongeza EACOP kwa kutekeleza suala hilo kwa ufanisi ambapo katika masaa zaidi Milioni Mbili waliyofanya kazi hakuna ajali iliyotokea kwenye maeneo yao ya kazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here