‘Tanzania ipo tayari kushirikiana na wadau kupambana na mabadiliko ya tabianchi’

0

SERIKALI imetoa wito kwa wadau wote kuendelea kuunga mkono jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kusisitiza iko tayari kushirikiana nao kuhakikisha Tanzania inakuwa yenye mazingira endelevu.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis wakati akifungua Jukwaa la Mazingira la ‘Tanzania Green Summit’ jijini Dar es Salaam mwishoni kwa wiki.

Alisema, athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo kupanda kwa joto, mvua zisizo na mpangilio, mafuriko, kupanda kwa usawa wa bahari na upotevu wa viumbe hai tayari vinaathiri maisha ya viumbe hai pamoja na maisha ya mwanadamu hivyo Jukwaa hilo ni fursa ya kukutanisha watendaji na wadau kujadili kisha kupata suluhisho.

Khamis alisema, tunapaswa kuunga mkono kuwainua wabunifu wanaobuni njia na miradi mbalimbali ambayo inaleta majawabu kuhusu changamoto za kimazingira na kuifanya Tanzania ya kijani.

Aidha, amebainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imechukua hatua za kimkakati kuweka uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira kuwa kipaumbele cha Taifa.

Naibu Waziri Khamis ametaja hatua hizo kuwa ni kuimarishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kanuni zinazoongoza matumizi endelevu ya ardhi, usimamizi wa rasilimali za maji, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti.

Hatua nyingine ni kujumuisha vipaumbele vya mabadiliko ya tabianchi na mazingira katika mikakati muhimu ya maendeleo ya taifa ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na Uongozi wa Tanzania katika nafasi za kimataifa na kikanda, kama vile uenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Richard Muyungi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here