Tanzania ina umeme wa kutosha – Dkt. Biteko

0

πŸ“Œ Asema ni jitihada za uwekezaji uliofanywa na Rais Dkt. Samia

πŸ“Œ Aipongeza TANESCO kwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania ina umeme wa kutosha hatua ambayo imechangiwa na kukamilika kwa Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambao pekee unazalisha Megawati 2115.

Naibu Waziri Mkuu ameyasema hayo Julai 10, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II ambapo amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO yapo baadhi ya maeneo yalikua na changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.

Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amefafanua kuwa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu TANESCO inatarajia kuongeza uzalishaji umeme katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1000 mpango wa sasa.

β€˜β€™Nataka niseme mbele yenu ndugu zangu, Mhe. Rais Samia ndio Kinara wa kufanya haya yote yafanikiwe amefanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati na ndio maana kwenye bajeti iliyopita Wizara hii imepata Shilingi Trilioni 2.3 kikubwa anataka wananchi wapate umeme wa uhakika,’’ alisema Dkt Biteko.

Aidha, Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.

β€˜β€™Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto za umeme lakini pia niwapongeze kwa kuimarisha Kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa bila gharama yoyote,’’ alisisitiza Dkt. Biteko.

Vilevile, Dkt. Biteko ametembelea Kituo cha Kupokea Gesi Asilia Kinyerezi kwa ajili ya kukagua miundombinu ya kusafirisha gesi na kuwataka kuongeza uzalishaji wa gesi ili kusaidia kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo katibu Mkuu wa Wizara ya nishati Mha. Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here