Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametangaza matokeo ya Sensa ya watu na makazi ambapo idadi ya watanzania imefika Milioni 61,741,120.
Rais Samia akitangaza matokeo hayo kwenye uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma alisema, watu 59,851,357 wapo Tanzania bara na watu 1,889,773 wapo Tanzania Zanzibar, pia kati ya watu 61,741,120 wanawake ni 31,687,990 sawa na asilimia 51 na wanaume ni 30,530,130 sawa na asilimia 49.
“Kwa mamlaka niliyopewa na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ninapenda kuwatangazia Tanzania ina idadi ya watu Milioni 61.741. Kati yao wanawake ni Milioni 31.6 sawa na asilimia 51 na wanaume Milioni 30.53 sawa na asilimia 49 ya watu wote,” alisema Rais Samia.
Rais Samia aliongeza: “Nataka niitangazie dunia kuwa Sensa ya watu na makazi ya 2022 imefuata vigezo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa. Tumeandika historia kwa mara ya kwanza tangu tupate uhuru, tumeweza kupata idadi ya majengo yote pamoja na anwani za makazi. Leo hii tumefika ukingoni mwa zoezi la sensa tulilofanya kwa ufanisi mkubwa. Sensa hii imefuata vigezo vyote vya Kimataifa.”
Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini, kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalumu.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, sensa ya mwaka 2022 ni ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012. Matokeo ya sensa ya mwaka 2012 yalionesha kuwa Tanzania ilikuwa na watu 44,929,002 wakiwamo 43,625,434 Tanzania Bara na 1,303,568 Zanzibari.