SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limetunukiwa tuzo ya hadhi ya juu katika kipengele cha waliosaidia kufanikisha na kurahisisha ukusanyaji wa kodi ngazi ya Taifa katika hafla ya siku ya utoaji tuzo kwa walipakodi bora kwa mwaka 2023/24.
Tuzo hiyo ambayo imekabidhiwa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye hafla iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kufanyika katika ukumbi wa Super Dome Masaki, jijini Dar es Salaam imeitambua TANAPA kama moja ya taasisi zilizosaidia kufanikisha na kurahisisha ukusanyaji wa kodi ngazi ya Taifa kwa mwaka 2023/2024.
Tuzo hiyo imekabidhiwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Yusuf Mwenda na kupokelewa kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moureen Mwaimale anayesimamia idara ya fedha TANAPA Makao Makuu.