TAKUKURU yafanya ufuatiliaji wa bajeti Kibaha DC

0

MAAFISA wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani wamefanya ufuatiliaji wa bajeti ya mwaka wa Fedha 2024/2025 ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Kikao kwa ajili ya ufuatiliaji huo kimefanyika Juni 5, 2025, kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa lengo la kubaini kama kuna mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato na kuangalia changamoto zinazokwamisha makusanyo.

Afisa wa TAKUKURU kutoka Mkoani, Ismail Ngoisa alisema, makadirio ya bajeti lazima yaende sambamba na makusanyo, ambapo aliipongeza Idara ya Biashara kwa mwenendo mzuri wa ukusanyaji wa mapato licha ya kuwepo kwa changamoto chache.

Awali, akifungua kikao hicho Afisa Utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Edward Masona aliwataka wakuu wa Idara kutoa taarifa za vyanzo vya mapato na kubainisha changamoto zilizokwamisha kufikia lengo la ukusanyaji.

Kwa upande wao wakuu wa Idara ya Ujenzi na Kilimo, Uvuvi na Mifugo wameombwa kuweka taarifa zao sawa hasa Mapato yatokanayo na Minada ya Mifugo sambamba na utoaji wa vibali vya ujenzi kwa Idara ya Ujenzi.

Kikao hicho cha ufuatiliaji kipo kwa mujibu wa Sheria 11/2007 kifungu 7(a) na (c) ya Sheria ya kuizuia na kupambana na Rushwa ambapo wakuu wa Idara wote na baadhi ya wataalamu walihudhuria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here