Tafiti zimebainisha kuwepo
kwa ukame – Dkt. Mwinyi

0

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema tafiti mbali mbali zinazoendelea kufanyika zinathibitisha mabadiliko ya tabia ya nchi husababisha kuwepo kwa vipindi vya ukame katika nchi mbali mbali duniani.

Dkt. Mwinyi alisema hayo katika Ufunguzi wa Kongamano la Maji la Kimataifa lililoendelea kufanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

Alisema, kuwepo kwa kiwango kikubwa cha joto pamoja na kukosekana mvua kwa kipindi kirefu pamoja na athari nyengine za kimazingira kunachangia kuwepo kwa changamoto kubwa ya ukosefu wa maji katika mataifa mbali mbai, ikiwemo Zanzibar.

Alisema, kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Ulaya (EEA) limebainisha kuwa wastani wa asilimia 20 ya Ardhi ya Bara la Ulaya linakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji kila mwaka,wakati ambapo asilimia 30 ya watu wa bara hilo wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji kila mwaka.

Akigusia kauli mbiu ya Kongamano hilo isimayo “Usimamazi endelevu wa rasilimali maji chini ya ardhi katika mabadiliko ya Tabia nchi, Dkt. Mwinyi alisema inaaakisi haja ya jamii kutunza vianzio vya maji, kwa kutambua athari za mabadiiko ya tabia nchi.

Alieleza kuwa, tatizo la upatikanaji wa maji linahusishwa na ukosefu au upungufu wa maji pamoja na changamoto za kisayansi na teknolojia na kubainisha namna upatikanaji wa maji unavyotegemea kuwepo kwa vianzio vya maji vya uhakika.

Alitumia fursa hiyo kuta wito wa kuhakikisha kunakuwepo mikakakati imara na endelevu ya kutunza vianzio mbali mbali vya maji viliyopo.

Alisema, Zanzibar itaendelea kutegemea upatikanaji wa maji safi na salama kutoka chini ya ardhi, hivyo akasisitiza usimamizi endelevu wa rasilimali maji chini ya ardhi.

Dkt. Mwinyi alisema, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya maji kwa kutekeleza miradi mikubwa kama ilivyopangwa na kuelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi wa CCM na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.

Aidha, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Shaibu Hassan Kaduara alisema, hivi sasa Wizara hiyo inatekeleza jumla ya miradi tisa katika sekta ya maji, na kusema miradi hiyo ikikamilika, shida ya maji waliyonayo wananchi wa Zanzibar itaondoka.

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph John Kilangi alisema, Kongamano hilo ni jukwaa la pekee litalotoa fursa nzuri kwa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kuwa na mtandao wa pamoja kwa lengo la kubadilishana mawazo na uzoefu.

Alisema, Kongamano hilo litatoa wito maalum kwa wataalamu na watafiti wa sekta ya maji kufanya mawasilisho ya tafiti zao ,ambapo jumla ya tafiti 57 zimepangwa kuwasilishwa.

Alisema, miongoni mwa tafiti hizo ni pamoja na ‘Ground water characteristic ina Zanzibar’ pamoja na Water demand Assessment in Zanzibar’.

Alisema, kongamano hilo linatambua mchango mkubwa wa vijana katika sekta ya maji, hivyo limeaanda zawadi kwa vijana mahiri watakaofanya vizuri katika uwasilishaji kwa lengo la kuwatia moyo na kuwajengea uwezo.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Maji Zanzibar Dkt. Salha Mohamed Kassim alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya maji kwa kuzingatia umuhimu wake katika maisha ya binadamu, maendeleo ya viwanda pamoja na kilimo.

Alisema, changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji hapa Zanzibar imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa huduma za kijamii katika vyanzo vya maji, ikiwemo makaazi pamoja na ongezeko kubwa la watu.

Aidha, akiwasilisha mada katika Kongamano hilo juu ya dhana ya uchumi wa Buluu Meneja Programu wa taasisi ya Western indian Ocean Marine Science Association (WIOMSA) Dkt. Valentine Ochanda alisisirtiza haja ya kuwepo ushirikianao kati ya Viongozi, watafiti pamoja na wafanyabiashara ili kuyawezesha Mataifa kunufaika na upatikanaji wa huduma za maji.

Kongamano hilo la siku limeandaliwa na Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kushirikiana na Global water partnership Tanzania (GWP TZ), taasisi ya SADC Ground water Monitoring Institute, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chuo Kikuu cha IHE-Delft cha nchini Uholanzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here