KATIKA nyanja mbalimbali, kauli mbiu huakisi hali halisi ya jamii, matarajio yake na mwelekeo wa maendeleo.
Kauli mbiu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele,” ni ujumbe mzito unaoleta tafakuri pana kuhusu maendeleo ya Tanzania kijamii, kiuchumi, na kiutawala.
Katika uchambuzi huu, nitatazama kauli mbiu hii kwa jicho la kichambuzi, nikichambua maana ninayoiona, uhusiano wake na jamii tunayoishi nayo, pamoja na umuhimu wake katika kujenga Tanzania yenye mshikamano na maendeleo endelevu.
KAZI – NGUZO YA MAENDELEO YA JAMII
Katika nadharia za maendeleo ya jamii, kazi ni msingi wa ustawi wa kiuchumi na kijamii. Max Weber, Mwanafalsafa mashuhuri, alieleza kwamba maendeleo ya jamii yanategemea mtazamo wa kazi. Katika muktadha wa Tanzania, ‘Kazi’ inaakisi:-
Mosi, Maendeleo ya Uchumi:- Taifa linalojikita katika kazi linazalisha mali, kuongeza uzalishaji na kukuza ajira.
Pili, Ujenzi wa Maadili ya Jamii:- Jamii inayothamini kazi hujenga nidhamu, kujituma, na uwajibikaji.
Kujenga uchumi wa kujitegemea ni lengo la msingi la Taifa, likiweka msingi wa heshima na ustawi wa wananchi.
Kwa hivyo, kauli mbiu hii inaendana na misingi ya maendeleo endelevu inayotambua kwamba kazi ni sharti la kujenga Taifa lenye tija.
UTU – MOYO WA JAMII ILIYO IMARA
Utu ni nguzo muhimu ya mshikamano na amani ya Kitaifa. Mwanafalsafa John Rawls alieleza kuwa jamii inayoendeshwa kwa misingi ya haki, usawa na utu huwa na mshikamano mkubwa na maendeleo ya kweli.
Katika muktadha huu, ‘Utu’ ndani ya kauli mbiu hii unamaanisha:- Mosi, maendeleo yenye uhalisia wa kibinadamu.Tanzania inahitaji maendeleo yanayozingatia siyo tu ukuaji wa uchumi, bali pia maisha bora ya watu kwa ujumla.
Pili, kuhimiza mshikamano wa Kitaifa. Taifa lenye utu hujenga mshikamano wa kijamii, likiepuka migawanyiko ya kikabila, kidini, na kiitikadi.
Kwa hivyo, kauli mbiu hii inaleta matumaini ya jamii inayothamini utu wa kila mwananchi, na kuweka mbele maslahi ya wengi badala ya wachache.
TUNASONGA MBELE – DHANA YA MAENDELEO ENDELEVU
Maono ya maendeleo inaeleza kuwa jamii haiwezi kukwama kwenye historia, bali lazima iendelee kusonga mbele kwa mabadiliko chanya. Kauli mbiu ya ‘Tunasonga Mbele’ ina maana kubwa katika:-
Mosi, kuendeleza mafanikio ya nyuma. Inasisitiza kuwa Taifa linasimama kwenye misingi iliyowekwa, lakini linalenga maendeleo zaidi.
Pili, kukabiliana na changamoto mpya. Dunia inabadilika, hivyo maendeleo lazima yazingatie mabadiliko ya kijamii, kiteknolojia, na kiuchumi.
Tatu, kuhamasisha mshikamano wa maendeleo. Inaonyesha kuwa maendeleo ni safari ya pamoja, yanayohitaji mshikamano wa serikali na wananchi.
Hii inaendana na mtazamo wa Mwanafalsafa Emile Durkheim, aliyesisitiza kuwa jamii inayosonga mbele ni ile inayojifunza kutoka kwa historia na kuhimiza mshikamano wa kijamii.
Kwa mtazamo wa Kisosholojia, ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’ ni kauli mbiu yenye uzito mkubwa kwa maendeleo ya Tanzania;- Inahimiza uchumi wa kujitegemea kupitia kazi, inalenga kujenga Taifa linalozalisha mali kwa bidii badala ya kutegemea misaada ya nje. Hii inaendana na mawazo ya Nyerere kuhusu kujitegemea.
Maendeleo yenye utu – Inasisitiza umuhimu wa kuwajali wananchi wote, bila kubagua. Hii ni hatua kubwa kuelekea usawa wa kijamii na haki kwa wote.
Mshikamano na umoja wa Kitaifa – Inahamasisha Watanzania kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa, badala ya kugawanyika kwa misingi ya kikabila, kidini au kisiasa.
Mabadiliko chanya kwa mustakabali wa Taifa – Inaonyesha kuwa maendeleo hayawezi kusimama; kila kizazi kinapaswa kuendeleza mafanikio yaliyopita kwa ari mpya.
Kwa kuhitimisha, kauli mbiu hii ni ya kupongeza kwa sababu inahamasisha uwajibikaji, mshikamano, na maendeleo jumuishi. Ni mwito kwa kila Mtanzania kujituma kwa bidii, kulinda utu wa kila mmoja, na kushiriki katika safari ya maendeleo ya Taifa letu.
Sasa, swali linabaki kwa kila mmoja wetu; Je, tuko tayari kuitafsiri kauli mbiu hii kwa vitendo?