Taasisi ya Uturuki yaipa Z’bar heshima ya kipekee

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Iyilik Dernegi kutoka nchini Uturuki kwa azma yake ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha kuandaa utekelezaji wa miradi yote kwa nchi za Afrika Mashariki.

Dkt. Mwinyi ametoa shukrani hizo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na ujumbe wa Taasisi ya Iyilik dernegi kutoka Uturuki, ulioongozwa na Kaimu Mwenyekiti wake Metin Calbay, ambapo pamoja na mambo mengine ulielezea juu ya shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo katika nchi mbali mbali Barani Afrika na Mashariki ya Kati.

Alisema, amefurahishwa na azma ya Taasisi hiyo ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu kwa miradi yote inayotekelezwa na taasisi hiyo kwa nchi za Afrika Mashariki, hivyo akasema Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kufanikisha azma hiyo.

Alisema, Serikali imepokea ombi la taasisi hiyo la kupatiwa eneo la Ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kitakachohusisha majengo ya skuli kuanzia ngazi ya maandalizi (Nursery) hadi Sekondari, chuo cha kilimo pamoja na chuo cha ufundi.

Alieleza kufurahishwa kwake na misaada mbali mbali inayotolewa na taasisi hiyo kwa jamii ya Wazanzibari na kote Barani Afrika, kwa kutambua kuwa jukumu hilo ni kazi ya Serikali. “Hii ni kazi ya serikali, lakini inapotokea taasisi ikasaidia wananchi …….tunashukuru sana.”

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi alishukuru na kupokea salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Kaka yake, kilichotokea hivi karibuni.

Mapema, Kaimu Mwenyekiti wa taasisi ya Iyilik Dernegi, Metin Calbay alisema taasisi hiyo ina azma ya kujenga kituo kikuu hapa nchini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kudumu katika nchi za Afrika Mashariki na hivyo akaiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupatiwa eneo hilo ili kufanikisha jambo hilo.

Alisema, ujenzi wa kituo hicho utahusisha majengo ya skuli kuanzia ngazi ya maandalizi (nursery) hadi elimu ya Sekondari, chuo cha kilimo, chuo cha ufundi na kubainisha kuwa mradi huo utaanza mara tu pale eneo hilo litakapopatikana.

Kaimu Mwenyekiti huyo alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kuwa, taaisisi hiyo tayari imewasaidia wananchi wa Zanzibar Mbuzi 450 wa Maziwa pamoja na kusaidia Mbuzi 1550 kwa ajili ya wananchi wa Tanzania Bara, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha kiuchumi.

Metin alisema, Taasisi ya Iyilik dernegi yenye makao makuu yake nchini Uturuki inajishughulisha na utoaji wa misaada katika nchi mbali mbali Barani Afrika, ikiwemo ya kugawa vyakula katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alisema, taasisi hiyo pia hutoa misaada katika uchimbaji wa Visima pamoja na kutoa misaada katika maeneo yanayokumbwa na majanga, ikiwemo vita.

Aidha, taasisi hiyo imefanikisha ujenzi wa nyumba na skuli kwa wakimbizi walioko katika maeneo yenye vita nchini Syria pamoja na kusaidia mbuzi Milioni tatu wa maziwa kwa nchi 25 Barani Afrika, ikiwa ni hatua kusaidia familia zenye maisha duni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here