Suala la usumbufu kwa wanachama NSSF kuwa historia

0
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba amesema, wanataka kuhakikisha huduma zote zinatolewa kwa njia ya mtandao ili kuwapunguzia usumbufu wanachama wao.

Mshomba alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioshirikisha wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa NSSF Mafao House Ilala, Dar es Salaam.

Alisema, NSSF inaendelea kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya TEHAMA na sasa shughuli nyingi za mfuko huo zinafanyika kupitia mifumo na kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2024/25, huduma zote muhimu zitatolewa kupitia mtandao.

“Kupitia mifumo ya TEHAMA, NSSF imewafikia kwa ukaribu wanachama na wadau wake, ambapo kwa sasa hawalazimika kufuata huduma ofisini badala yake wanazipata huko huko waliko na hivyo tumewaondolea adha ya kufuata huduma umbali mrefu,” alisema Mshomba.

Aliendelea kusema, wanataka kuhakikisha suala la usumbufu kwa wanachama wao linakuwa historia “mtu mwenye miaka 70 ni usumbufu kumuweka muda mrefu, tunajisikia vibaya sana. Tukifanikisha kwa asilimia 100% itatusaidia kutoa huduma vizuri.”

Mkurugenzi huyo alisema, NSSF imezindua mfumo unaomuwezesha mwanachama kufungua madai ya mafao kwa njia ya mtandao na lengo ni kumrahisishia kupata huduma karibu zaidi bila ya kufika katika ofisi za NSSF.

“Mfumo huu utaondoa kabisa usumbufu kama ulikuwepo na pia utawawezesha wanachama wetu tunaowahudumia kupata huduma kwa wakati, kwa kuwa mifumo hii ni wazi na ufuatiliaji unakuwa rahisi,” alisema Mshomba.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa NSSF Masha Mshomba, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mfuko huo.

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na wanachama katika Mfuko tofauti na kipindi cha nyuma na kupelekea thamani ya Mfuko kufikia Trilioni 8.5 tofauti na Trilioni 4.8 wakati alipokuwa anaingia madarakani,” alisema Mshomba na kuongeza kuwa, watahakikisha wanaboresha zaidi huduma zao, kuwa waadilifu na kuendelea kutoa elimu kwa wateja wao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here