Simba, Yanga na uhusiano
na bendi maarufu za taarabu

0

Na Yahya Msangi

NILIFIKA Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 1968. Kusema kweli nilikuja kwa kaka yangu Ahmad bila kumpa taarifa. Nilikuja na treni, nilipofika nikaulizia yalipo Makao Makuu ya TANESCO, nikaelekezwa na nilifika.

Hapo nilikutana na mlinzi ambaye nilimuuliza kama mwenyeji wangu yupo, naye alinijibu, ‘huyo saa hii yuko ‘computer room,’ subiri akitoka nitamwambia upo hapa.’ Kweli baada ya saa moja kaka akaja mbio, akashangaa nilivyokuja ghafla. Basi akanipeleka kwenye chumba cha Kompyuta nikashangaa, ilikuwa imejaa ukuta mzima.

Kazi ya chumba hicho ilikuwa ni kuchapisha risiti za wateja, enzi zile kompyuta za mezani na mpakato hazikuwepo wala hazijagundulika. Nilikaa mahali hapo hadi saa mbili usiku, zamu yake ikaisha tukaenda alipokuwa anaishi maeneo ya Magomeni Mwembe Chai; tulipanda basi la ghorofa. Enzi zile lilikuwa linafanya safari zake Feri, Ilala na Magomeni.

Tilipofika akaniuliza kama nyumbani niliaga, nikakiri kwamba nimeondoka bila kuaga, kwani ningeaga nisingepata ruhusa. Basi alicheka sana kaka yangu yule, Mungu amrehemu! Basi nikamwambia sikutaka mechi ya Yanga na Asante Kotoko inipite! Nakumbuka nilifika Jumatano, mechi ilikuwa inachezwa Jumapili inayofuata. Basi kaka akaniambia tutakwenda. Nikajua naam, nimeingia mjini!

Basi, kwa mara ya kwanza nikatazama mechi live! Yanga dhidi ya Asante Kotoko (The Porcupines of Kumasi – Kakakuona wa Kumasi Ghana). Ngoma ikalala droo! Enzi za akina golikipa Mensah (Kotoko) na Michael Elias ‘snake.’

Sasa nikupe historia Simba na Yanga. Timu hizi zilianzishwa miaka ya 1930 na waliojiita watu wa Pwani; wazaramo, wadengereko na waarabu. Kama ulitoka Rombo au Mwika hata ungejua vipi kutembea juu ya mpira hawakupi namba. Vilabu hivi vikafanya mahusiano na vikundi vingine vya wenyeji fani mbalimbali, lakini maarufu zaidi vikundi vya muziki wa taarabu.

Huko nako mtu ambaye sio mtu wa Pwani, hata angekuwa na sauti nzuri kama chiriku isingekuwa rahisi kupewa nafasi ya kuimba. Yanga wao wakashirikiana na ‘Egyptian Music Group’ na Simba ‘Alwatan Musical Group.’ Ni baada ya muda kupita vilabu hivi vikafungua milango kwa ambao sio watu wa Pwani.

Pia, siasa ya nchi hazikuruhusu waendeleze huu ubaguzi. Basi kufika miaka ya 70 vilabu hivi vikaingia mitafaruku ya kutisha, mgogoro wa Simba ulianzishwa na watu wawili; Joachim Kimwaga ambaye alikuwa Afisa Magereza na mwenyeji wa Tabora na Jimmy Ngonya aliyekuwa karani Shirika la Bima la Taifa.

Hawa walianzisha harakati za kutaka uongozi Simba. Waliungwa mkono na wanachama wengi na wakafanikiwa kutwaa uongozi. Wakafukuza wanachama 70 ambao waliunga mkono uongozi uliopinduliwa. Hawa wanachama 70 na uongozi uliopita wakaamua kuanzisha klabu yao ikaitwa ‘Red Stars,’ lakini wakambiwa waipe jina la kiswahili ikaitwa Nyota nyekundu.

Ila wachezaji wakaamua kubaki Simba na uongozi mpya. Haraka sana ‘Alwatan Music Group’ wakahama Simba na kwenda ‘Red Stars’.

Nyota nyekundu kalazimika kusajili wachezaji wapya. Mmoja ni Rosta Ndunguru, mchezaji aliyekuwa mtata sana. Huyu Rosta tulicheza naye mpira kule Geita sisi tukiwa Pamba Sports yeye akiwa Kurugenzi Sports. Alikuwa mgumu kama nondo usipokaa sawa anakuvunja mguu.

Basi siku Nyota nyekundu ikicheza na Simba, ndio ilikuwa vita. Ndunguru mwenye umbile dogo sana na Kina Sabu ‘dubu’, Jumanne ‘masiminti’ na Martin Kikwa, Kajole ‘machela’! Ndunguru yeye hajali umbo la mtu. Huyu Martini Kikwa yeye tulicheza naye mpira yeye akiwa Kibohehe Secondary na mimi KNCU Secondary.

Tukijumuika kombaini ya sekondari mkoa wa Kilimanjaro na kina Idi Juma (alikuwa Mawenzi Secondary) na Sam Kampambe (alikuwa Moshi Technical). Ilikuwa kombaini matata sana. Wote hawa sasa ni marehemu.

Kwa upande mwingine Yanga nako kukazuka mgogoro, chanzo kikuu ni safari ya Yanga Lagos Nigeria kupambana nadhani na Enugu Ranges ya kina Emmanuel Okala (kipa matata sana). Yanga ilikuwa na wachezaji haswa, Magwiji kwelikweli. Sasa walivimba vichwa. Wakadai kocha Tambwe Leya anawadharau na anawasimamia kama watoto.

Waliporudi wakaanza mgomo baridi kushinikiza Tambwe afukuzwe. Mara likazuka kundi likiongozwa na mfanyabiashara David Mwambungu likadai Mangara Tabu Mangara anafuja mali za Yanga. Wakadai anakingiwa kifua na Shiraz. Mzee Mangara ni mmoja wa walioanzisha klabu ya Yanga na ndiye alianzisha ujenzi wa jengo la klabu na Kaunda Stadium.

Enzi zile hakuna klabu nyingine Afrika iliyokuwa na jengo na kiwanja chake, lakini mfadhili mkuu alikuwa Shiraz. Tajiri aliyekuwa na viwanda. Kwa kuhadaiwa na kwa kuendeleza mgogoro kati yake na kina Mzee Mangara na Shiraz Tambwe, akaamua kujiunga na kundi la akina Mwambungu.

Siku zote Tambwe alikuwa anadai marupurupu zaidi na zaidi akiamini yeye ndio aliiinua kiwango cha klabu hiyo. Japo ni kweli, lakini alikuta msingi mzuri ulioachwa na Profesa Victor. Vurugu likawa kubwa kukazuka kambi mbili; Kambi ya Mangara na Shiraz ikiwa Mtaa wa Mafia Kariakoo, ambapo ndiko yalikuwa makao makuu ya kwanza ya Yanga na kambi ya Mwambungu na Tambwe iliyokuwa Kaunda Stadium.

Ikabidi TANU na Serikali ziingilie kati, lakini wakagoma kufika mwafaka. Ndipo Mkuu wa Mkoa (nadhani Mzee Songambele) akaamuru mkutano wa uchaguzi ufanyike. Mzee Mangara akakataa kugombea na watu wa kambi yake waliogombea wakashindwa vibaya kwenye kura. Wachezaji karibu wote wakakataa kucheza chini ya Tambwe Leya na uongozi mpya ukawafukuza.

Mangara na Shiraz wakataka kusajili klabu mpya kanuni zikawarudi. Wakaamua wachezaji waende klabu ya Nyota Afrika iliyokuwa Morogoro. Nyota Afrika, Toto Afrika ya Mwanza na African Temeke na African Sports (Tanga) zilikuwa kama matawi ya Yanga.

Inasemekana mjadala ulizuka waende Tanga au Mwanza ikaonekana waende Morogoro, badaye Nyota Afrika ilihamia Dar es Salaam na ikabadili jina ikaitwa Pan Africa. Haraka sana na ‘Egyptian Musical Club’ wakahama Yanga wakaenda Pan. Kati ya viongozi wa kwanza Serikalini kuhama Yanga na kujiunga na klabu hiyo ni Hayati Benjamin William Mkapa. Hii ndio sehemu ya historia ya hivi vilabu viwili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here