SIDO yatoa msukumo mpya Tanga

0

Na Angela Msimbira, Tanga

MAAFISA waandamizi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Tanzania Bara na Zanzibar, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa kimataifa, wamefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Tanga kwa lengo la kujifunza na kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Green and Smart Cities unaotekelezwa kupitia programu ya IncluCities kwa usaidizi wa Enabel.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulijionea namna Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) linavyotoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya wakazi wa Jiji la Tanga, hasa wanawake na vijana, kupitia mafunzo ya ujuzi, ushauri wa kitaalamu, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya teknolojia vinavyowezesha uongezaji thamani wa bidhaa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mratibu wa Mradi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Tanzania Bara, Shabani Ghuhia, alisema wamejionea kwa vitendo utekelezaji wa sera ya serikali ya kujenga miji jumuishi yenye uchumi shirikishi, kwa kupitia taasisi kama SIDO.

“SIDO imeonyesha mfano wa namna taasisi za ndani zinavyoweza kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa kawaida. Huu ni mfano bora wa mafanikio ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Serikali na mashirika ya kimataifa,” alisema Ghuhia.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa kwa ujumbe huo, zaidi ya wajasiriamali 400 watanufaika na mafunzo ya kiufundi, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia rafiki katika shughuli zao, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji, kupanua masoko ya bidhaa za ndani, na kuchochea matumizi ya mbinu bunifu zinazozingatia mazingira.

Aidha, ziara hiyo imekuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kuhusu utekelezaji wa sera na programu za maendeleo ya miji, pamoja na kutathmini namna bora ya kupanua miradi hiyo kwa mikoa mingine nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here