Siasa za wivu, upotoshaji na uongozi uliopitwa na wakati

0

KATIKA siku za hivi karibuni, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dkt. Wilbrod Slaa ameibuka tena na kauli zinazotilia shaka dhamira yake halisi katika siasa za Tanzania.

Kupitia jukwaa la ‘kumekucha,’ amejaribu kutetea msimamo wa Chadema wa ‘No Reform, No Election’ akidai kuwa si suala la kususia uchaguzi, bali wananchi wenyewe wataamua kuuzuia. Kauli hizi kwa mtazamo wa wengi, ni propaganda tupu zinazolenga kuwapotosha wananchi na kujenga mazingira ya hofu na mgawanyiko katika Taifa.

Hata hivyo, wananchi wa Tanzania wanaelewa kuwa siasa si mchezo wa vitisho na fujo, bali ni uwanja wa hoja, sera, na utekelezaji. Chadema kupitia kauli za Dkt. Slaa na viongozi wengine wa chama hicho, wanajaribu kuonyesha kuwa, uchaguzi hauwezi kufanyika bila mabadiliko wanayoyataka wao, wakibeza jitihada za maboresho yaliyofanyika katika sheria za uchaguzi.

Tunaelewa kuwa, upinzani wa kweli ni ule unaojiandaa kushindana kwa hoja na kushinda katika uwanja wa demokrasia, si ule unaotafuta visingizio vya kukwepa uchaguzi kwa sababu tayari wanajua hawana uwezo wa kushinda.

Historia inaonyesha kuwa, Watanzania ni watu wenye busara na hawawezi kushawishika na propaganda za hofu zinazosukumwa na Chadema.

Wakati CCM inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kuboresha miundombinu, na kuimarisha uchumi wa nchi, Chadema wanapoteza muda wao wakihubiri woga na migogoro isiyo na manufaa kwa wananchi.

Ukiwasikiliza wananchi huko mitaani na kwenye mitandao ya kijamii wanahoji. Kama Chadema wanadai kuwa wao ndio sauti ya watu, kwa nini wanaogopa uchaguzi? Je, wanajua kuwa hawana ushawishi tena kwa wananchi, ndiyo maana wanatafuta njia za kuzuia uchaguzi?

Pamoja na mambo mengine, kujitokeza kwa Dkt. Slaa kuwasaidia Chadema, nako kunaongeza mdororo wa chama hicho kilichowahi kuwa ngome ya upinzani nchini kufikia malengo yake.

Kwasasa, Dkt. Slaa hana ushawishi tena kama ilivyokuwa miaka ya nyuma baada ya kupotea kwa muda mrefu, alidhani anaweza kurudi na kusukuma propaganda zile zile za zamani. Tanzania imebadilika. Wananchi wameelimika. Wanajua kuwa siasa za sasa si za kutumia hofu na chokochoko, bali ni siasa za maendeleo na ustawi wa taifa.

Kauli yake kuwa wananchi ndio watakaozuia uchaguzi ni dharau kwa wananchi wenyewe. Anawafanya waonekane kama chombo cha kufanikisha malengo ya chama badala ya kuwa wananchi wenye haki zao binafsi. Ukweli ni kwamba, Watanzania wana malengo yao ya maendeleo na hawawezi kupoteza muda wao kufuata kauli za kisiasa zisizo na mashiko.

Mataifa yote yanayoendesha siasa za kidemokrasia yana mfumo wa uchaguzi wa wazi. Hakuna taifa duniani linaloruhusu chama kimoja kutunga masharti ya kufanyika kwa uchaguzi. Chadema wanaposema ‘No Reform, No Election,’ wanajiona kama wao ndio wamiliki wa mchakato wa uchaguzi, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya demokrasia.

Katika mfumo wa kidemokrasia, chama kinachotaka kushinda lazima kijipange, kijiimarishe, na kishawishi wananchi kwa sera zake. Lakini Chadema wanatafuta njia rahisi—kususia, kulalamika, na kutisha watu; wanajua wazi kuwa hawawezi kushinda kwa sanduku la kura.

  1. Wakati Chadema wanajihusisha na siasa za migogoro, CCM inaendelea kujenga nchi. Miradi mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, na uboreshaji wa huduma za afya na elimu ni ushahidi kwamba, Serikali ya CCM inatekeleza maendeleo kwa vitendo.

Wananchi wanaona tofauti kati ya chama kinachofanya kazi kwa ajili ya maendeleo na chama kinachotafuta visingizio vya kisiasa kila kukicha. Wananchi wa Tanzania wanahitaji maendeleo, si siasa za vurugu na visingizio.

Katika demokrasia, uchaguzi ni haki ya wananchi, si mali ya chama fulani. Chadema wakiamua kususia, ni wao watakaopoteza, si wananchi. Tanzania itaendelea mbele na uchaguzi utafanyika kama kawaida.

Dkt. Slaa na viongozi wa Chadema wanapaswa kuelewa kuwa siasa za vitisho na hofu hazina nafasi tena. Watanzania ni watu wenye akili timamu, wanajua wanachotaka, na hawawezi kupotoshwa na propaganda za upinzani.

Watanzania wamechagua maendeleo, na wataendelea na uchaguzi bila kujali maneno ya hofu kutoka kwa wanaotafuta visingizio vya kushindwa. Uchaguzi utafanyika, na Tanzania itaendelea mbele.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here