SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeendelea kutekeleza kwa mafanikio mpango wa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa walimu, ambapo hadi kufikia Desemba 2024 jumla ya walimu 3,798 kutoka shule 1,791 za msingi na sekondari za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar wamepatiwa mafunzo hayo.
Mafunzo yamekuwa yakitekelezwa kila mwaka tangu mwaka wa fedha 2016/17, yamelenga kuwajengea walimu uwezo wa kutatua matatizo madogo madogo ya vifaa vya TEHAMA vilivyotolewa na UCSAF katika shule zao.
Kupitia utekelezaji wa mradi huu, Serikali imefanikiwa kuongeza ufanisi katika matumizi ya TEHAMA kwenye shule za Serikali, jambo linalochangia kuinua ubora wa elimu na kukuza ujuzi wa kidijitali kwa wanafunzi na walimu.
Mafunzo haya yamekuwa yakifanyika kwa ushirikiano na taasisi za elimu ya juu ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa Kanda ya Kati, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa Kanda ya Mashariki na Pwani.











