Na Georgina Misama, MAELEZO
SERIKALI imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuimarisha sekta ya maji nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama, ambapo katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Maji la Kidunda.
Akizungumza jijini humo katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Maji Kigamboni, Rais Samia Suluhu Hassan alisema, Serikali inatambua kuwa mradi wa maji wa Kigamboni ni wa kupunguza makali ya changamoto hiyo na kwamba suluhisho la kudumu litatokana na mradi wa Bwawa la Kidunda ambalo litakapokamilika na kujazwa maji litaweza kuhudumia Jiji la Dar es Salaam kwa miaka mitatu mfululizo.
Rais Samia alisema, bwawa hilo lenye thamani ya Shilingi Bilioni 329 litakalojengwa kwa kutumia fedha za ndani litawezesha kuwepo uhakika wa maji kwa kipindi cha mwaka mzima jijini Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani ambayo kwa sasa yanategemea maji ya Mto Ruvu.
Ujenzi wa bwawa hilo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu 2022 mpaka 2025 ambapo utakapokamilika utachochea kasi ya maendeleo ya viwanda katika mkoa wa Pwani pamoja na Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, mradi wa maji wa Kigamboni utaimarisha huduma ya maji katika maeneo ya Temeke, Ilala na Kinondoni hivyo kupunguza ukali wa mgao wa maji.
Hali kadhalika, Rais Samia ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha inasambaza maji kwa wananchi katika wilaya ya Kigamboni kwa asilimia 100.
Rais Samia ameitaka Wizara ya Maji kutoa elimu kwa wananchi kuacha kuchoma misitu ovyo, kuchepua maji pamoja na kuingiza mifugo hasa wananchi wanaoishi kando ya vyanzo vya maji kwani vitendo hivyo husababisha upungufu wa maji.
“Uwepo wa Bwawa hili umeongelewa kwa muda mrefu, lakini leo ninayo furaha ya kwamba hatimaye sasa tunakwenda kujenga, tena kwa kutumia fedha zetu za ndani, mkataba tayari mkandarasi amekabidhiwa na leo mkandarasi atakwenda kuonyeshwa eneo litakapojengwa bwawa hilo ambalo tunatarajia litachua miezi 36 hadi likamilike,” alisema Rais Samia.