Serikali yatoa siku nne huduma za mwendokasi kurejea maeneo yote Dar

0

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe ametoa muda wa siku nne kuhakikisha huduma ya mabasi ya mwendokasi inarejea katika maeneo yote ya mkoa wa Dar es Salaam ili kuwawezesha wananchi kuendelea kunufaika na usafiri huo.

Maelekezo hayo yametolewa wakati wa uzinduzi wa safari za mabasi hayo kutoka Ubungo Maji hadi Gerezani baada ya huduma hiyo kusimama tangu Oktoba 29, 2025 kufuatia vurugu zilizojitokeza kwenye baadhi ya maeneo ya mkoa huo ikiwemo uharibifu wa vituo vya mabasi hayo.

Uzinduzi huo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba aliyeelekeza kurejeshwa kwa huduma hiyo ndani ya siku 10 na kwa mujibu wa Prof. Shemdoe utekelezaji huo umefanikiwa ndani ya siku sita pekee.

“Mhe. Waziri Mkuu alituelekeza ndani ya siku 10 tuwe tumekamilisha marekebisho ya muda kutoka hapa Gerezani hadi Kimara, Leo nina furaha kusema kwamba ndani ya siku sita tumeweza kusogeza huduma hii hadi Ubungo Maji.” amesema Prof. Shemdoe.

Ameeleza kuwa maeneo mengine yaliyoharibika ikiwemo Kimara, Magomeni na Morocco yanaendelea kufanyiwa ukarabati kwa ushirikiano kati ya DART, UDART, TANESCO na TANROADS huku akisisitiza umuhimu wa huduma hiyo kurejea kikamilifu ndani ya siku nne zijazo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here