Serikali yatoa onyo kwa wanaoendelea kuzalisha mifuko ya plastiki

0

SERIKALI imetoa onyo kali kwa watu na kampuni zinazoendelea kuzalisha bidhaa za mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na kuingiza katika matumizi kwa njia za panya.

Imesema, itaendelea kufanya doria za kushtukiza katika viwanda, viwanda bubu na masoko ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wote wanaojihusisha na biashara hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema hayo leo Mei 27, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitakuwa jijini Dodoma na mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hatua hiyo inakuja kutokana na kujitokeza kwa changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya tubings kutumika kama vibebeo na vifungashio ambavyo havina sifa na kutokukidhi matakwa yaliyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kufuatia hatua, Mhandisi Masauni amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mamlaka nyingine za umma kuendelea kufuatilia na kuwabaini wahusika wote wanaokiuka sheria na kuzalisha bidhaa za plastiki zilizopigwa marufuku kuzalishwa na kutumika nchini.

“Niwakumbushe Watanzania wenzangu kuzingatia maelekezo ya Serikali kuachana na mifuko ya plastiki na kutumia mifuko mbadala ambayo kwa sasa inapatikana nchini kote kwa gharama nafuu” amesisitiza Mhandisi Masauni.

Aidha, alisema kuwa pamoja na changamoto hiyo, kwa kiasi kikubwa Tanzania imepiga hatua katika kudhibiti taka za plastiki baada ya kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni, 2019, hatua iliyosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu kutambua mifuko na vifungashio vya plastiki vilivyoruhusiwa, Masauni alisema kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma sambamba na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa mifuko mbadala ambazo ni rafiki kwa mazingira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here