Serikali yatangaza neema kwa wahandisi wanawake

0
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kutoa fursa kwa Wahandisi Wanawake kushiriki kikamilifu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja nchini.

Ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 840 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya ambapo kazi hizo zitatekelezwa na Makandarasi na Wahandisi Wazawa wakiwemo Wanawake.

Bashungwa amezungumza hayo Agosti 21, 2024 Mkoani Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la tisa (9) la Wahandisi Wanawake lililoandaliwa na Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), kupitia Kitengo cha Wanawake na kuwasisitiza Wahandisi Wanawake kuchangamkia fursa hizo.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa Wazawa na hivyo kupitia Mkakati wa Wizara ya Ujenzi wa wakushirikisha Wakandarasi na Wahandisi Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya barabara (Local Content), unatoa vipaumbele na fursa katika kuwahusisha Wahandisi Wanawake kikamilifu katika kutekeleza dhana ya ushirikishwaji katika miradi endelevu ya kimkakati na uwekezaji nchini”, alisema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa kila mwaka Serikali imekuwa ikitenga fedha takribani Bilioni 600 kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara ambapo zinatoa fursa kwa makundi maalum ikiwemo Kundi la Wanawake kutekeleza kazi hizo kwa asilimia 100.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara ya Ujenzi imetenga miradi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 120 za lami ambazo zitashindanishwa kwa Makandarasi wa ndani pekee na zitatoa kipaumbele kwa Wakandarasi wanawake pamoja na ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 20, ambao umegawanyika katika sehemu 4 za Kilometa tano tano.

Kadhalika, Bashungwa ametoa wito kwa Taasisi ya Wahandisi Tanzania kupitia Kitengo cha Wahandisi Wanawake kuweka mikakati ya kuhamasisha na kuwahusisha wanafunzi watoto wa kike kuanzia ngazi ya Shule ya Msingi kujiamini na kujiunga na masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia Julai 2024, Tanzania Bara ina wahandisi 38,233 ambapo kati ya hao wanawake ni 5,006, sawa na 15.07%.

Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaunga mkono jitihada zinazoendelea kufanwa ili kuhakikisha idadi ya wanawake na wasichana katika mambo ya ubunifu na ubobezi wa kisayansi inaongezeka ambapo hilo limedhihirishwa na kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaosoma sayansi katika sekondari, vyuo vya amali/VETA, vyuo vya kati na vyuo vikuu sambamba na ujenzi wa Shule maalum za sayansi kwa wasichana kwa kila mkoa.

Naye, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhandisi Zena Said ametoa wito kwa Wahandisi Wanawake kujiamini, kushirikiana kwa pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali kutoka Sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitengo cha Wanawake kutoka Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Mhandisi Rehana Juma ameeleza kuwa Kitengo hicho kilianzishwa kwa lengo la kuendeleza kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi ya Wahandisi Tanzania pamoja na kuhamasisha wanawake kujiunga na fani ya Uhandisi, Sayansi na Hesabu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here