Serikali yapokea Bilioni 45.5 kutoka NMB

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa Hundi ya Shilingi Bilioni 45.5 (Gawio la Serikali) kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Benki ya NMB yaliyofanyika Mlimani City, Jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB Dkt. Edwin Mhede pamoja na Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu wakishuhudia.

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika yote ya umma kujiendesha kwa ufanisi, tija na ushindani ili yaweze kuwa endelevu.  

Rais Samia ametoa tamko hilo wakati wa hafla ya benki ya NMB ya kukabidhi gawio kwa Serikali na kusherehekea miaka 25 ya safari ya mafanikio ya benki hiyo, iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Rais Samia alisema Serikali inaendelea kufanya tathimini ya utendaji wa mashirika yote ya umma na yale ambayo Serikali ina hisa kubwa ili kubaini mashirika yasiyo na faida yanayoshindwa kujiendesha na kuitia hasara Serikali.

Alisema, tathimini hiyo inafanywa na Msajili wa Hazina ambapo Serikali itayachukulia hatua na kuyafuta mashirika ambayo hayafanyi vizuri, kuyasaidia na kuyapa miongozo ya namna ya kujiendesha ili yapate faida.

Rais Samia amewataka wajasiriamali, wakulima na wananchi wote wanaohudumiwa na benki ya NMB kuendelea kuwa waaminifu wanapochukua mikopo bila dhamana ili benki hiyo iendelee kuwa na ustawi.  

Benki ya NMB imekabidhi gawio la Shilingi Bilioni 45.5 ambapo Serikali inamiliki 31.8% ya hisa katika benki hiyo huku asilimia zingine zikiwa zinamilikiwa na wadau kutoka sekta binafsi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Benki ya NMB wanaohudumu tangu kuanzishwa kwake mara baada ya kufunga maadhimisho ya miaka 25 ya Mafanikio  ya Benki hiyo  Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here