Na Mwandishi wa OMH
SERIKALI ya Tanzania, kupita Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), na Kampuni ya Perseus Mining Limited, zimesaini rasmi mkataba wa nyongeza wa umiliki wa hisa katika Mradi wa Dhahabu wa Nyanzaga, hatua inayochukuliwa kuwa ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
Mkataba huo uliosainiwa Agosti 20, 2025 katika hafla iliyofanyika katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza, unaongeza umiliki wa Serikali, kupitia OMH, kutoka asilimia 16 hadi 20 katika Kampuni ya Ubia ya Sotta Mining Corporation Limited, ambayo inasimamia utekelezaji wa mradi mkubwa wa dhahabu unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Perseus na Serikali.
Mkataba huo ulisainiwa na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, kwa upande wa Tanzania, na Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus, Lee-Anne de Bruin, mbele ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Mchechu alisema, nyongeza ya hisa inaashiria dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania kwa njia endelevu na ya uwajibikaji.
Mchechu pia alieleza kuwa usainiaji wa mkataba huo umetokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Serikali na wawekezaji, na kwamba Serikali itaendelea kutengeneza mazingira rafiki ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unafanikishwa kwa mafanikio makubwa.
Kwa upande wake Waziri wa Madini, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alieleza kuwa mkataba huo ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa Serikali na Kampuni binafsi katika sekta ya madini.
Aidha, alisema mradi huo utaongeza ajira, mapato ya Serikali, na huduma za kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Sengerema na taifa kwa ujumla.
“Utekelezaji wa Mradi wa Dhahabu wa Nyanzaga utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Leo tunahakikishia Watanzania kuwa mradi huu utaendeshwa kwa manufaa yao,” alisema Waziri Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa zaidi ya Sh1 trilioni zinatarajiwa kuwekezwa kwenye mradi huo, na kwamba Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wake kwa karibu kuhakikisha wananchi wanapata fursa za ajira, ushiriki wa wananchi kupitia huduma na bidhaa, na mapato makubwa kupitia kodi na gawio la hisa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Perseus, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha mazungumzo na kusaini mkataba huo wa nyongeza unaowezesha kuanza uzalishaji mwanzoni mwa mwaka 2027.
“Tunamshukuru Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia yaliyochangia mafanikio haya,” alisema Lee-Anne.