Na Clement Robert, WAF – Dar es Salaam
SERIKALI imeendelea kuimarisha juhudi za kukuza uzalishaji wa dawa nchini kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kufikia kujitegemea katika upatikanaji wa dawa na kuboresha huduma za afya nchini.
Akizungumza katika kikao na wadau wa viwanda vya dawa leo Machi 23, 2026 kwenye ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya dawa na vifaa tiba Emmanuel Tayari amesema serikali bado imejidhatiti kusaidia wazalishaji wote wa dawa nchini na ipo tayari kushirikiana nao kutatua changamoto zinazowakabili.
Kikao hicho kimemkutanisha Tayari na Mwenyekiti wa kampuni ya Tanzania Phamathetical Manufacturing Association (TPMA) Bashir Haroon ambapo wamejadili njia bora za kuongeza kasi ya uzalishaji wa dawa nchini.
Tayari amesema dhima ya serikali ni kuhakikisha sekta ya afya inafikia malengo ya kujitegemea katika uzalishaji wa dawa kwa kiwango cha kujitosheleza ili kutimiza maono ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya.
“Tutahakikisha mazingira yanakuwa rafiki kwa wazalishaji wa dawa ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuchangia kikamilifu maendeleo ya sekta ya afya. Dhamira ya Serikali ni kuona nchi inajitegemea katika upatikanaji wa dawa, hatua itakayosaidia kuboresha huduma za afya na kufikia malengo ya kitaifa” amesema Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya dawa na vifaatiba.