Serikali yadhamiria kumaliza migogoro ya ardhi

0

Na. OMM, Rukwa

SERIKALI ya Awamu ya Sita imedhamiria kumaliza migogoro ya ardhi iliyopo na kuweka utaratibu endelevu wa kudhibiti migogoro mipya ili wananchi waendelee na shughuli za maendeleo bila vikwazo.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri (8) wa Wizara za Kisekta inayoshugulikia utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 Mashimba Ndaki, mjini Sumbawanga.

Waziri Ndaki amebainisha kuwa, tangu Kamati hiyo ilipoanza kazi mwaka 2019 tayari imepatia ufumbuzi migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 920 vilivyoanishwa kuwa migogoro ya ardhi kati ya vijiji 975 ambapo migogoro katika vijiji 55 vilivyosalia kazi ya ufuatiliaji inaendelea chini ya Kamati ya wataalam

“Tayari vijiji 920 kati ya vijiji 975 vyenye migogoro ya ardhi ikihusisha mashamba, uvamizi wa maeneo ya hifadhi, mapori na au, mipaka tayari Serikali imetoa maelekezo ya utatuzi wake”alisema Waziri Ndaki.

Akielezea utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika mkoa wa Rukwa, Waziri Ndaki alisema jumla ya vijiji (13) vilianishwa kuwa na migogoro ya matumizi ya ardhi ambapo tayari vijiji (12) vimetolewa uamuzi na Baraza la Mawaziri aidha kubaki au kufanyiwa marekebisho ya mipaka na kuwa kijiji kimoja kati ya hivyo kinaendelea kufanyiwa kazi na kamati ya wataalam.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga aliishukuru Serikali kwa kazi nzuri ya kufuatilia utatuzi wa migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa, atahakikisha maelekezo yaliyotolewa na Kamati ya Mawaziri wa wizara za kisekta atayasimamia ili yatekelezwe kikamilifu.

Kamati hiyo ya Mawaziri inahusisha Wizara za Mifugo na Uvuvi, OR- TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maji, Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Wizara ya Maliasili, Wizara ya Ulinzi ,Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Kilimo.

Baadhi ya mapendekezo ya kamati kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni kubakisha vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa wananchi na kuhakiki pamoja na kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.

Pia, yapo mapendekezo ya kumega baadhi ya hifadhi na kugawia wafugaji na wakulima, kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya ardhi, kupitia upya sheria ya vyanzo vya maji inayozungumzia mita 60 na kufutwa kwa mashamba yasiyoendelezwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here