Serikali yaanza kutenga fedha za ujenzi wa Uwanja wa Mpira Dodoma

0

Na Shamimu Nyaki – Dodoma

NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul ameeleza, ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu jijini Dodoma upo katika hatua ya utekelezaji na tayari Serikali imeshaanza kutenga fedha za ujenzi huo.

Gekul ameeleza hayo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge Innocent Edward Kalogeris ( Morogoro Kusini) aliyeuliza ni lini ahadi ya ujenzi wa Uwanja wa mpira Dodoma iliyotolewa na Mfalme wa Moroko itatekelezwa.

Akijibu swali hilo, Gekul alisema, mawasiliano kuhusu utekelezaji wa mradi huo baina ya Serikali ya Tanzania na Morocco yanaendelea, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau na wabia wa maendeleo.

“Serikali imeshakamilisha upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi huo, na mwaka huu wa fedha ujenzi utaanza, lakini pia kutakua na kiasi chaShilingi Bilioni 10 kuboresha viwanja vya michezo vya Arusha, Tanga, Dodoma na Geita” alisema Gekul.

Waziri wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa ametoa majibu ya nyongeza katika swali hilo kwa kusisitiza, ujenzi huo utakua wa kisasa na miondombinu bora ambayo inaendana na teknolojia ya viwanja vya sasa Duniani.

Akijibu swali la nyongeza la Salma Kikwete kuhusu kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa Majaliwa Stadium, Gekul alisema Serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za wadau wanaowekeza katika Sekta ya michezo, ambapo imepunguza kodi katika nyasi bandia pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wawekazaji wa sekta hiyo.

Gekuk ametumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa kwa ujenzi wa Uwanja wa Ruangwa na kueleza kuwa ujenzi huo utakua chachu ya kuongeza vipaji katika Soka, na kupunguza changamoto ya miundombinu ya viwanja nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here