MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kusimamia kwa dhati na kwa haki misingi ya demokrasia.
Alisema, watahakikisha wananchi wanatumia haki yao ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi kwa uhuru, kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuchagua viongozi wenye sifa wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote hususan vijana kuwa waangalifu na watu wasioitakia mema nchi kwa kuepuka kutumiwa vibaya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Makamu wa Rais alisema, Wadau wote wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa wanahimizwa na kukumbushwa kuwa wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika katika hali ya amani na utulivu, kwa kuendesha kampeni zenye staha na kuzingatia Sheria na miongozo mbalimbali ya uchaguzi.
Aliongeza, Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 42(2) na 65, Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024 pamoja na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 4 ya mwaka 2018.
Halikadhali Makamu wa Rais ameagiza Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, ili waweze kutekeleza jukumu la kizalendo walilokabidhiwa la kuhakikisha kuwa wanawafikia wananchi na kuwapa taarifa sahihi kuhusu sera, mipango, miradi na mikakati ya Serikali katika kuwaletea Maendeleo.
Vilevile, Makamu wa Rais amesema Mbio za Mwenge pamoja na mambo mengine zitaangazia masuala ya lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhini ya VVU na UKIMWI, mapambano dhidi ya dawa za kulevya pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.