Serikali kuwasomesha vijana masomo ya nyuklia nje ya nchi

0
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof. Lazaro Busagala (Picha na Francis Dande).

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Awamu Sita kupitia Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission – TAEC) ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mpango wa ufadhili kwa vijana wa kitanzania kusoma masomo ya teknolojia na sayansi ya nyuklia katika ngazi ya shahada za uzamili.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Lazaro Busagala katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Prof. Busagala alisema, kila mwaka vijana watanzania watano watapata ufadhili huo, ambapo lengo ni kuongeza idadi ya wataalam nchini katika nyanja ya teknolojia na sayansi ya nyuklia ili kuhakikisha nchi inanufaika ipasavyo na fursa za taaluma hiyo.

Mbali na mpango huo, alisema Serikali pia imekuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo wa kitaalam watumishi wake ili kujenga taifa lenye uwezo katika teknolojia ya nyuklia.

“Kwa kufuata mpango wa mafunzo uliowekwa na kuanza kutekelezwa, TAEC imeshasomesha 29 na inaendelea kusomesha wengine 32 ndani ya miaka mitatu, jumla itakuwa watumishi 61,” alisema.

Aidha, aliongeza mbali na mafunzo hayo, Serikali katika utekelezaji wa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya 2003, imefanikiwa kusajili wataalam wa mionzi 788 wenye sifa za kutoa huduma ya mionzi kwa watu.

“Ndani ya miaka mitatu, Serikali imesajili wataalum 1,289 wa kutoa huduma ya mionzi kwa wagonjwa, kutengeneza, kukarabati na kuendesha vifaa vya nyuklia, jambo hili lilikuwa halifanyiki kwa kipindi cha nyuma,” alisema Prof. Lazaro Busagala.

Prof. Busagala alitumia mkutano huo kuwataka wananchi kuchangamkia fursa za Sayansi na Teknolojia ya nyuklia katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuitumia kwa usahihi bila kuleta madhara kwa wananchi na mazingira kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here