Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kwenye bajeti ijayo, Serikali inatarajia kutenga fedha zitakazotumika na Mfuko maalum ambao utaanzishwa kwa ajili ya Mpango wa miaka 10 wa kuhakikisha nchi inahamia kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Rais Samia alisema hayo wakati wa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia linalofanyika kwa siku mbili, kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Alisema, akiwa Makamu wa Rais alianzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani, ambapo kampeni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo hivi sasa Serikali inalenga kumtua mama mzigo wa kuni na kulinda mazingira ya nchi.
“Bajeti ijayo itengwe fedha ya kuanzisha Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia, lengo ni kumtua mama mzigo wa kuni kichwani. Nikiwa Makamu wa Rais niliweka lengo la kumtua mama ndoo kichwani, nina furaha kusema kwamba, nimetimiza kwa asilimia 80, ukiacha hizi athari za mabadiliko ya tabia ya nchi na ukame unaotuandama,” alisema.
Rais Samia alisema, ni lazima waangalie namna ya kumpunguzia mwanamke mzigo na madhara ya kutumia nishati isiyo salama, kwani analazimika kutembea umbali mrefu kuifuata, lakini mbali na hilo, anapata madhara kutokana na kutumia nishati isiyo salama.
“Twende na Nishati Safi ya Kupikia, tuwapunguzie wanawake mzigo na madhara,” alisisitiza Rais Samia na kuongeza kuwa, mwanamke akipata nishati safi karibu na eneo analoishi, itakuwa rahisi kufanya shughuli za kiuchumi, kwani atapata muda wa kutosha.
Aidha, ili kufanikisha hayo, Rais Samia aliagiza kuundwa kwa Kikosi Kazi ambacho kitatoa dira kwa Taifa ambayo itaiongoza Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutafuta suluhu ya Nishati Safi na endelevu ya Kupikia. “Nitajisikia fahari ikifika 2032 Tanzania hii iwe na nishati ya kupikia kwa asilimia hizo hizo 80, 90 kama sio zote,”
Alisema, suala la kufikia malengo ya kuachana na Nishati sio suala la muda mfupi na linahitaji kuwekewa mikakati, kwani takwimu zinaonyesha kuwa, hivi sasa kaya zinazopikia kwa kutumia mitungi ya gesi ni asilimia 5, umeme asilimia 3 na nishati nyingine safi asilimia 2.2.
“Hii inaonyesha bado kuna kazi ya kuhamasisha matumizi ya nishati iliyo safi na salama. Tunapaswa kuwa na mkakati madhubuti wa kisera na kibajeti pamoja na kuweka mazingira wezeshi katika kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati safi.”
“Kwenye hili Serikali peke yetu hatuwezi tunapaswa kwenda sambamba na sekta binafsi, nashukuru baadhi yao wameanza kujitokeza tunakwenda nao sambamba lakini si kisera kwa sababu ni fursa ya biashara hivyo kuna haja ya kuwa na sera inayoshughulikia suala hili,” alisema Rais Samia.
Mbali na hilo, Rais Samia aliagiza taasisi zote ambazo zinahudumia watu kuanzia 300, watumie Nishati safi ikiwemo gesi, na alitoa mwaka mmoja kwa Wizara ya Nishati kusimamia utekelezaji huo. “Wizara wajielekeze kuhakikisha taasisi kubwa zinatumia nishati safi ya kupikia, 2024 nisimame kwa wananchi niseme nimeweza kufanya hili.”