Serikali kufungua mawasiliano Simanjiro

0

SERIKALI kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inajipanga kufungua mawasiliano kwa kuunganisha Barabara ya Langa-Mkuu na Msitu wa Tembo katika Kata ya Msitu wa Tembo- Ngorika kuelekea Ngange wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Naftari Chaula amesema hayo wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa ujenzi na matengenezo ya barabara wilayani humo.

Mhandisi Chaula alisema, Barabara hiyo imekuwa ikikumbwa na mafuriko pamoja na sehemu nyingine kutofunguliwa kutokana na kuwa na makorongo mengi yaliyosababishwa na mvua nyingi.

Alisema, kwa mwaka huu wa fedha wanatarajia kukamilisha ujenzi wa madaraja kwa zaidi ya asilimia 70 na tayari mkandarasi yupo eneo la ujenzi akiendelea na uchimbaji na upangaji wa mawe na kwamba kukamilika kwa ujenzi huo kutafungua mawasiliano kati ya Kata ya Ngorika na Msitu wa Tembo na kuwezesha usafirishaji wa mazao ya uvuvi kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu.

“Wananchi wamekuwa wakipata shida sana katika shughuli za usafirishaji wa mazao ya uvuvi, bidhaa nyingine za kilimo na hata wananchi wa Ngorika kwenda Hospitali ya Kata ya Msitu wa Tembo na Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro na mahali kwingine kwaajili ya matibabu” alisema Mhandisi Chaula.

Kwa upande wao wananchi wa Kata hiyo wameishukuru Serikali kupitia Wakala hiyo kwa kuwapelekea mradi huo ambao wanasema utasaidia kuondoa changamoto walizokuwa wakikutana nazo.

Thomas Sokoine Mkazi wa Kijiji cha Londoto Kata ya Msitu wa Tembo alisema, kujengwa kwa daraja katika korongo hilo kutasaidia wananchi wakiwemo watoto kutokukwama tena kuvuka upande wa pili.

Kwa upande wake Robert Juma dereva wa lori la mizigo alisema, barabara hiyo imekuwa changamoto hususani wakati wa mvua na kumshukuru Rais Samia kwa kuwapelekea mradi huo wa ujenzi wa makalavati ambao anaamini utawaondolea kero wanayokumbana nayo ikiwemo kusitisha shughuli za usafirishaji hasa katika kipindi cha mvua.

Naye Jorum Yohana Mkazi wa Msitu wa Tembo alisema maeneo yao yalikuwa ni hatarishi kutokana na maji kuleta adha kubwa kwa wananchi na kuishukuru Serikali kwa kuwawekea lami kipande cha Kilometa 1.

Aliongeza kuwa, Serikali imeongeza fedha kwa kuwajengea makalavati, hivyo wanaamini barabara hiyo ikikamilika itawasaidia katika shughuli za kilimo, ufugaji na biashara zitaendelea kuinuka na hivyo kupata unafuu wa kimaisha na kuweza kuwainganisha kati ya Mkoa wa Manyara na Kilimanjaro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here