Na Albert Kawogo
RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Elimu la Kimataifa (GPE), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo ongezeko la ufaulu na idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu.
Kikwete ameyasema hayo Julai 14, 2025, kwenye Shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam, wakati Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), Malala Fund na Global Partnership for Education (GPE), walipotembelea Shule hiyo kukagua mabweni ya wasichana na wenye uhitaji maalum yaliyojengwa na Serikali ya Tanzania.
Dkt. Kikwete alisema, katika utawala wake kipaumbele kikubwa kwenye sekta ya elimu ilikuwa ni kuhakikisha watoto wa kike na kiume wana haki ya kusoma, ndio maana kulikuwa na mwitikio mkubwa wa watoto kwenda shule.
Pia, walihakikisha elimu ya Awali, Msingi Sekondari mpaka Chuo Kikuu ni haki ya msingi kwa kila mtoto, jambo ambalo viongozi waliofuata baada ya utawala wake, wamekuwa wakiliendeleza akiwemo Hayati Dkt. John Magufuli na sasa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Rais Mstaafu aliongeza kuwa, Duniani kote watoto wapatao Milioni 272 hawaendi shule, huku Afrika ikitajwa kuchangia idadi kubwa ya watoto kukosa Elimu.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa ongezeko kubwa la wanafunzi kuanzia ngazi ya awali, msingi na sekondari, ambapo taarifa zinaonyesha kuwa, tangu kuanza kwa elimu bure mwaka 2016, idadi imeongezeka kufikia Milioni 3.
Naye, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga alisema, mabadiliko ya mitaala yamejenga mazingira salama na Jumuishi kwa wanafunzi wote, hasa wasichana na wenye mahitaji maalum huku akisisitiza kuwa, teknolojia ya Kidijitali na matumizi ya Akili mnemba (Artificial Intelligence – AI) sasa ni sehemu ya mitaala, na serikali inaendelea kuhimiza ushiriki wa wasichana kwenye masomo ya TEHAMA na STEM.
Kwa upande wake Malala Yousafzai, Mwanzilishi wa Malala Fund, amesifu juhudi za Tanzania katika kuwawezesha wasichana kupata elimu, huku akitoa wito kwa jamii kuungana kuhakikisha wasichana hawakatishi masomo yao.