Na Rashid Mtagaluka
KATIKA muktadha wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kulijenga taifa kupitia sekta ya kilimo sekta inayochangia takribani 26.7% ya Pato la Taifa (GDP) na kutoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania.
Wiki iliyopita, akiwa ziarani Mkoani Kagera, Dkt. Samia alikutana na maelfu ya wananchi na kuzungumza kwa kina kuhusu mustakabali wa kilimo cha kahawa, zao la kimkakati kwa uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Kiukweli Kagera, ambayo huzalisha zaidi ya 50% ya kahawa yote nchini, imeendelea kuwa eneo la kimkakati katika ajenda ya kilimo cha kisasa.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia alieleza kwa kina kuhusu mikakati ya Serikali kupitia mpango wa “Kilimo ni Biashara”, ambao unalenga kuleta mapinduzi ya kijani kwa kuwageuza wakulima kuwa wajasiriamali wa kisasa.
Kwa kujibu wa Dkt Samia, dhamira kuu ni kukigeuza kilimo kutoka kuwa shughuli ya kujikimu hadi kuwa chanzo thabiti cha ajira, kipato, na maendeleo ya kiuchumi.
Ukipitia takwimu mbalimbali, utagundua kwamba, mkoa wa Kagera umejipambanua kwa miaka mingi kama kinara wa uzalishaji wa kahawa bora nchini Tanzania, hasa aina ya Arabica na Robusta.
Kwa mfano takwimu kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), mwaka 2023/24 mkoa huo unaosafirisha kahawa hadi kwenye masoko ya nje kama Japan, Ujerumani, Marekani na Italia, na kuchangia mamilioni ya dola katika mapato ya kigeni, ulizalisha zaidi ya tani 56,000 za kahawa, sawa na zaidi ya nusu ya uzalishaji wa kitaifa.
Hata hivyo, sekta hii muhimu inakabiliwa na changamoto sugu kama vile ukosefu wa miche, bora, mabadiliko ya tabianchi, bei ya chini ya soko la dunia, miundombinu hafifu ya uchakataji na masoko na kutegemea zana duni kama jembe la mkono.
Kwa kuwa Dkt. Samia, anazifahamu kwa kina changamoto hizi, amesisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuwekeza katika taasisi za utafiti wa miche bora ya kahawa, usambazaji wa pembezoni bora, na uimarishaji wa vikundi vya ushirika ili kuhakikisha wakulima wanapata bei ya haki.
Aidha, kupitia mpango huu mpya, serikali inalenga kuwashirikisha vijana na wanawake kwa kiwango kikubwa zaidi. Kwa mfano, Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 308 kwa mwaka 2025/26 kwa ajili ya kugharamia upatikanaji wa pembejeo, mafunzo ya kilimo, na vifaa vya kisasa kupitia ruzuku au mikopo nafuu.
Vilevile zaidi ya matrekta 800 yanatarajiwa kusambazwa kwa wakulima wadogo na vikundi vya vijana katika maeneo ya kimkakati kama Kagera, Mbeya, na Ruvuma, mikoa inayotambulika kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya kibiashara.
Katika sekta ya kahawa, miche bora ni nyenzo muhimu kwa uzalishaji endelevu. Dkt. Samia ameeleza kuwa serikali kwa kushirikiana na taasisi za utafiti kama Tanzania Coffee Research Institute (TaCRI) itaongeza uzalishaji wa miche ya kisasa inayostahimili magonjwa na ukame. Lengo ni kuzalisha zaidi ya miche Milioni 20 ifikapo mwaka 2026.
Vilevile, uwekezaji mkubwa unafanywa katika kuongeza thamani ya kahawa kwa kujenga viwanda vidogo vya uchakataji, kupanua masoko ya ndani na nje, na kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu ubora wa daraja la kahawa, ambao ndio msingi wa kupata bei ya juu sokoni.
Kwa zaidi ya miaka 60, kilimo nchini Tanzania kimekuwa kikifanywa kwa kutumia jembe la mkono, hali iliyosababisha tija duni na mavuno yasiyoridhisha. Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zaidi ya asilimia 70 ya wakulima bado wanatumia jembe la mkono.
Dkt. Samia anataka kuondoa hali hii kwa kuimarisha upatikanaji wa trekta, mashine za kunyunyizia dawa, na vifaa vya kisasa vya kupalilia na kuvuna, kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja na ushirika wa wakulima.
Na kama utajipa utulivu wa kuisikiliza kwa makini hotuba ya Dkt. Samia aliyoitoa pale mkoani Kagera utaona kuwa, haikuwa tu sehemu ya kampeni, bali ni ahadi ya matumaini na uthibitisho wa uongozi wenye maono. Dkt. Samia anaonesha kuwa anaelewa siasa ya maendeleo ni siasa ya utekelezaji na si maneno matupu.
Kwa kutoa kipaumbele kwa kilimo cha kahawa, Dkt. Samia anachochea mabadiliko ya kweli katika maisha ya mamilioni ya Watanzania. Uwekezaji katika miche bora, zana za kisasa, elimu ya kilimo, na viwanda vya kuongeza thamani ni hatua madhubuti kuelekea uchumi jumuishi unaotegemea kilimo cha kisasa.
Kagera iko katika ramani ya maendeleo. Na chini ya uongozi wa Dkt. Samia, kuna kila dalili kwamba mkoa huo utaendelea kuwa nguzo kuu ya kahawa bora siyo tu kwa Tanzania, bali kwa Afrika Mashariki na masoko ya dunia.