Samia afunika nyanda za juu, amaliza kazi

0

Na Albert Kawogo

MGOMBEA wa Urais chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kama vile alikuwa haamini umati mkubwa wa watu waliofika kumsikiliza katika mikutano yake ya kampeni, huku watu hao wakiwa watulivu na wenye furaha kumsikiliza.

Baada ya kumalizana na Kanda ya Mashariki inaundwa na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro na kutembelea baadhi ya majimbo ya mkoa huo, moja kwa moja alitua Songwe.

Songwe ni mkoa mpya unaounda Nyanda za juu Kusini pamoja na mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa ambayo ukiondoa Rukwa ambao hakwenda, ina jumla ya wakazi Milioni 4.88.

Dkt. Samia baada ya kuanza na Songwe kwa kishindo, Septemba 3, 2025, amehitimisha kampeni hizo Septemba 7, 2025 kwa kishindo kama alivyoanza huku Uwanja wa Samora ukiwa umetapika.

AWEKA HISTORIA

Mgombea huyo wa Urais ameweka historia Kanda ya Nyanda za Juu, tangu alipoingia Septemba 3, 2025 kwenye mji wa Songwe na hadi alipohitimisha Septemba 7, 2025 amehitimisha Iringa Mjini.

Katika mikutano yake iliyovuta maelfu, akiwa Makambako amesema kutokana na umati unaojitokeza kwenye mikutano yake yote, na kama ingekuwa hiyari yake, angeenda kutulia Ikulu lakini inamlazimu kuomba kupanda jukwaani kuomba kura na kuinadi Ilani.

Mbunge wa Isimani, William Lukuvi alisema kwenye moja ya mikutano kuwa wanaIringa wanajazana kwenye mikutano kwa ajili ya shukurani kwani mengi Rais Samia ameyatekeleza.

HESABU ZA CCM

Ukiangalia kampeni za chama hicho ambazo zimepigwa kwa hesabu kali, CCM ilianza kusaka kura Kanda ya Mashariki ambapo alifanya uzinduzi wa kampeni.

Kanda ya Mashariki inaundwa na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro. Ni mkoa huo pekee wa Morogoro ameutembelea.

Mkakati wa Rais Samia na Mgombea mwenza, Dkt. Emmanuel Nchimbi wameanza na Kanda za Ushindi. Kanda zinazoweza kuamua kura kutokana na wingi wa wakazi.

Kwa pamoja walikuwa kwenye Uzinduzi wa Kampeni jijini Dar es Salaam, lakini baada ya hapo wakatawanyika; Rais Samia Nyanda za Juu na Dkt. Nchimbi kwenda Kanda ya Ziwa.

Kanda ambazo CCM imeanza nazo, ziko kwenye tatu bora za idadi ya watu. Kanda ya Ziwa inayoundwa na mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga na Mara na ndiyo Kanda yenye idadi kubwa ya watu kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022. Kanda hiyo ya Ziwa ina watu 16,687,560.

Dkt. Nchimbi alikuwa na kazi moja, kuinadi ilani ya uchaguzi, lakini pia kumuombea kura, Rais Samia Suluhu Hassan.

Ujumbe umefika kwani kila alipokuwa anapita au kuandaliwa mikutano rasmi, maelfu ya wapenzi, wanachama na mashabiki wa CCM walikuwa wakijitokeza kwa wingi.

SONGWE HADI IRINGA

Rais Samia aliingia Nyanda hizo akitokea kanda ya Mashariki yenye watu Milioni 12.6 na baadaye Songwe, Mbeya Njombe na Iringa. Mikoa hiyo kipekee ina watu wapatao Milioni 4.88 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi 2022.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa mji huo unaokua kwa kasi, Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa ameahidi ujenzi wa barabara ya TANZAM inayounganisha Tanzania na Zambia.

Anasema kuwa Serikali itajenga barabara za njia nne kuanzia Igawa hadi Tunduma, ikiwa ni urefu wa Kilomita 70 kwa ajili nya kupunguza msongamano wa malori katika barabara hiyo.

Akiwa mwenye tabasamu, anasema kuwa maboresho na uwekezaji yamefanyika Bandari ya Dar es Salaam na kwa sasa inafanya kazi kwa ufanisi hivyo mzigo umeongezeka na kuna kila sababu ya kuitengeneza miundombinu hiyo.

Mgombea huyo urais amesema dhamira yake ni kujenga barabara za kiwango cha lami katika wilaya zote za mikoa ili kuziunganisha na Makao Makuu ya mikoa.

Mbali na hilo, Dkt. Samia amewaahidi Watanzania kujenga madaraja ili kupunguza changamoto zinazotokana na kutokuwepo kwa vivuko.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Vwawa mkoani Songwe Jumatano Septemba 3,2025 amesema madaraja yote barabara ndani ya miaka mitano wanakwenda kujenga.

‘’Lengo letu ni kuunganisha wilaya zote na makao makuu ya mikoa kwa kiwango cha lami. Hii kazi inaendelea kufanyika, tutaendelea kuifanya hadi tuhakikishe wilaya zote Tanzania zimeunganishwa kwa barabara za lami na makao makuu ya mikoa.’’

Kuhusu umeme, Dkt. Samia amewahakikishia wananchi wa Songwe kuwa kazi kubwa imefanyika kujenga njia ya Kilovati 730 ya kusafirishia umeme kutoka Iringa hadi mkoa huo.

“Kati ya Kilovati 730, Kilovati 400 zitatumika katika mikoa mitatu ukiwamo wa Songwe, zilizobaki tutauza kwa majirani zetu (Zambia). Huu ndio mpango wetu ndani ya mitano, mbali na kuiunganisha Songwe katika gridi ya Taifa, lakini tunahitaji kujenga njii hizi.”

Akiwa Rungwe amesema, lengo ni kuhakikisha wanatekeleza yote yanayowagusa wananchi moja kwa moja, ikiwemo umeme, maji, elimu, huduma za afya, barabara na mengine mengi.

Aidha, Samia amesema, wanafanya mpango wa kuvipa nguvu vyama vya ushirika ikiwemo kuvikabidhi mashamba ya chai kutoka kwa walioshindwa kuyaendeleza.

Amesema, Serikali itayachukua mashamba yote ya chai ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza na kuyakabidhi vyama vya ushirika.

Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mufindi mkoani Iringa waliojitokeza kwenye mkutano huo, amesema hiyo inaonyesha imani kubwa ya wananchi wa Mufindi kwa viongozi wao.

Amesema Serikali itafanyia tathmini mashamba yote ya chai mkoani Iringa ambayo hayaendelezwi na itayakabidhi kwa vyama vya ushirika ili kuyaendeleza.

Rais Samia anayetetea nafasi yake, amesema kuwa Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha mashamba hayo yanaendelezwa.

Akifafanua zaidi kuhusu mashamba hayo ya chai, Rais Samia amesema Makampuni ya Mufindi Tea & Cofee yaliomba mashamba hayo lakini inaonekana wameyumba hivyo mchakato wa kuyachukua utafanyika.

Amesema chai ni zao litaendelezwa kwa kuwa ni la asili na la siku nyingi na hawawezi kuacha mtu mwingine awaharibie.

Huku akishangiliwa na maelfu ya wapenzi, mashabiki na wanachama wa CCM, amesema, Serikali itatafuta masoko na itatajirika kwa kupata fedha kutokana na chai.

Kuhusu barabara, amesema ujenzi wa Kilomita 40.4 umeanza kwamba kazi imeanza kufanyika na itakamilika kama ilivyopangwa pamoja na barabara ya Kasanga-Igowole-Igo ya Kilomita 54.5 na yenyewe itafanyiwa kazi.

Kuhusu mashine za X-ray, amesema Serikali itapeleka kwenye Hospitali za wilaya ili wananchi wapate huduma bora.

Akiwa Makambako, mgombea huyo amesema endapo watapata ridhaa, ndani ya muda mfupi watafungua vituo vya kununulia mahindi katika mkoa wa Njombe.

Aidha, amewataka watendaji Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kurekebishe mifumo yao ya kodi huku akisema wameunda Tume ya kuangalia hali ya Makambako na ripoti itakayokuja itawaongoza kuona jinsi ya kuweka kituo kimoja cha kikodi.

Kuhusu Bandari kavu, wataangalia waone wapi panafaa kwa bandari na watafanyia kazi ripoti kwani tayari Songwe, Mbeya na Njombe wote wametaka bandari kavu kwa hiyo ukitoa Songwe ambayo ilishapita, wataangalia wapi panafaa kujengwa Bandari Kavu.

Akiishambulia Nyanda za Juu Kusini kwa kumwaga sera, mgombea huyo akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali Katibu Mkuu Dkt. Asha-Rose Migiro, Katibu wa itikadi na uenezi Kenan Kihongosi, wajumbe wa kamati kuu, NEC na viongozi wa mkoa wilaya, alitumia nafasi hiyo kuwanadi wagombea wa nafasi ya ubunge katika majimbo yote ya Mkoa wa Iringa wakiwemo udiwani.

Samia ambaye alifunga kazi katika mikutano yake takribani yote kwa kukusanya maelfu ya mashabiki, wapenzi na wanachama wa CCM kuanzia Songwe hadi Iringa mjini, alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi na viongozi wa Iringa kwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza.

Kabla ya kutoa ahadi mbalimbali, amewakumbusha wananchi kuhusu miradi mbalimbali iliotekelezwa na Serikali yake ndani ya miaka mine huku akiwaomba kuwaomba wamchague ili kuwaletea maendeleo.

Akizungumzia kuhusu nishati ya umeme Dkt. Samia amesema kuwa sekta ya nishati ameifanyia mageuzi makubwa ambapo uzalishaji wa umeme umeongezeka kwa kiasi kikubwa, na katika kipindi kifupi cha miaka minne Serikali yake imesambaza umeme katika mitaa na vijiji nchi nzima.

Hatua iliobakia sasa ni kumalizia kusambaza umeme katika vitongoji vilivyosalia, na kusema kuwa serikali yake inampango wa kuongeza vyanzo vya uzalishaji wa umeme kutoka iliyopo sasa hadi Megawati 8000 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wa wafanyabiashara, amesema katika siku 100 za uongozi wake sekta hii inajumuisha mama lishe, maafisa usafirishaji (bodaboda) atairasimisha huku akiahidi kujenga jengo la kisasa la Machinga Complex katika mji wa Iringa ili kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo kufanya biashara zao katika mazingira mazuri.

Kuhusu viwanda mkoani Iringa, Dkt. Samia amesema kuwa licha ya ongezeko la viwanda kutoka 24 mwaka 2020 hadi 40 mwaka 2025 , Serikali yake itapochaguliwa itahakikisha inajenga kongani ya viwanda katika wilaya ya Iringa ili kuongeza ajira kwa vijana na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, misitu na madini.

Kwa upande wa kilimo, amesema endapo atapewa ridhaa, Serikali yake itaendelea kuwekeza katika kilimo ili kuwainua wakulima katika maeneo mbalimbali ya nchi wakiwemo wa Iringa.

Amesema kipindi kilichopita, mkoa wa Iringa umenufaika na miradi ya kilimo ikiwemo kilimo cha umwagiliaji ambapo wilaya ya Iringa pekee ilinufaika na miradi mikubwa tisa ya skimu ya umwagiliaji yenye thamani ya Shilingi Bilioni 104.4 kwa wakulima 62,800 mkoani Iringa.

Aidha, Dkt. Samia amesema kuwa serikali yake imetekeleza mradi wa umwagiliaji wa Mtula katika halmashauri ya Mafinga kwa thamani ya Shilingi Bilioni 566.

Amesema kipindi kilichopita, mkoa wa Iringa umenufaika na miradi ya kilimo ikiwemo kilimo cha umwagiliaji ambapo wilaya ya Iringa pekee ilinufaika na miradi mikubwa tisa ya skimu ya umwagiliaji yenye thamani ya Shilingi Bilioni 104.4 kwa wakulima 62,800 mkoani Iringa.

Dkt. Samia pia amesema kuwa Serikali yake imetekeleza mradi wa umwagiliaji wa Mtula katika halmashauri ya Mafinga kwa thamani ya Shilingi Bilioni 566.

Upatikanaji wa ruzuku ya mbolea umewawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali. Ameahidi kuwa endapo watamchagua katika uchaguzi mkuu ujao serikali yake itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima.

Aidha, ameahidi kuwa Serikali itajenga vituo 50 vya kuhifadhia mazao ya parachichi sambamba na vituo vya kuhifadhia mazao ya mbogamboga, vilevile amewahidi wananchi wa Iringa kuwa endapo atachaguliwa atajenga maghala ya kuhifadhia mazao ya biashara na chakula katika mkoa wa Iringa

Sambamba na hilo, Dkt. Samia ameahidi kuanzishwa vituo vya ukodishaji wa zana za kilimo ili wakulima wapate huduma za kilimo kwa bei nafuu kwa kuwa Serikali itatoza nusu ya bei inayotozwa na sekta binafsi.

Akizungumzia sekta ya ujenzi na uchukuzi Dkt. Samia amesema Serikali yake imefanya jitihada nyingi katika sekta hii muhimu kwa uchumi wa watu wa Iringa ambapo Uwanja wa Ndege wa Nduli sehemu kubwa ya ujenzi umekamilika na tayari huduma mbalimbali zinapatikana ikiwemo ndege za Shirika la Ndege ATCL na mashirika mengine zinatua.

Kuhusu kupunguza msongamano katika mji wa Iringa Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya mchepuko (bypass) ambapo ujenzi upo asilimia tano na utakamilika katika kipindi cha 2025-2030.
Dkt. Samia amegusia ujenzi wa Daraja la Kitwiru-Isakalilo ambapo amesema litakamilishwa katika kipindi kijacho cha awamu ya uongozi wake.

Pia, amegusia ya kwamba amepokea maombi mengi yaliyotolewa na wagombea ubunge hasa ya ujenzi wa Barabara za lami, ambapo amesema amezichukua na atazifanyia kazi katika kipindi cha pili cha uongozi wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here