Na Mwandishi Wetu
WAKATI baadhi ya wanaharakati na wapinzani wakizua taharuki kwa kuhusisha Serikali, Jeshi la Polisi na tukio la kupotea kwa Padri Cammilius Nikata wa Jimbo Kuu Katoliki Songea na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino – (SAUT) Mwanza, imebainika suala hilo halina chembe yoyote ya utekaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 11, 2025 na askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea Mhashamu Damian Denis Dallu, Padri Nikata aliondoka katika nyumba ya Mapadri iliyopo Songea wakati akijiandaa kurudi katika kituo chake cha kazi Mwanza baada ya kutoka kwenye Mafungo Dodoma.
Siku chache baadae, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, SACP Marco Chilya alitoa taarifa ya kupatikana kwa Padri Nikata, ambapo alisema Oktoba 17, 2025 alikutwa kwenye mashamba ya Kijiji cha Mawa, wilayani Namtumbo akiwa amedhoofika.
Kamanda Chilya alisema, upelelezi umebainisha chanzo cha tukio hilo la Padri Nikata kutokomea mashambani karibu na kijiji alichozaliwa, ni pamoja na Msongo wa Mawazo uliotokana na Madeni mengi yaliyokuwa juu ya uwezo wake.
Pia, msongo huo ulisababishwa na mahusiano baada ya kuachwa na mpenzi wake aliyekuwa naye takribani miaka tisa ambaye kwa kipindi chote alikuwa akimuhudumia kwa gharama kubwa, ambapo kipindi cha mwezi Juni hadi Septemba imebainika, alimuhudumia mpenzi wake kiasi cha Shilingi 39,158,000 kwa kutoa kwenye akaunti yake ya CRDB.
Sababu nyingine, Kamanda alisema Padri Nikata alikuwa na maradhi ya muda mrefu, ambapo anasumbuliwa na presha ya macho na alifanikiwa kufanyiwa Operesheni ya jicho moja “na sasa alikuwa anahitajika kufanyiwa Operesheni ya jicho la pili, lakini alikosa pesa kutokana na matumizi makubwa yakumuhudumia mwanamke wake.”
Sambamba na hilo, Kamanda Chilya alisema Padri huyo alikuwa ameamua kuachana na kazi ya upadri kwa sababu za kiafya, mahusiano na hali mbaya ya kifedha, lakini hakupewa nafasi ya kusikilizwa na uongozi wake.
Alisema, hali ya Padri Nikata inaendelea kuimarika baada ya kupata huduma ya kwanza katika Hospitali ya Rufaa Songea – Homso huku Jeshi la Polisi likidhibitisha kuwa Padri Camillus Aron Nikata hakutekwa, bali alijipoteza yeye mwenyewe kutokana na Msongo wa Mawazo na sababu zilizotajwa hapo awali.
Kutokana na tukio hilo, watu mbalimbali wamekuwa na maoni tofauti huku wakiwasihi watanzania kuwa na utulivu pindi yanapotokea matukio ya aina hiyo na kuepuka kutoa hukumu kwa kusikiliza maneno ya mitandaoni kutoka kwa watu ambao wana nia ovu na amani ya nchi.
Walisema, wanapaswa kujua kwamba, watu ambao wanachochea chuki kwenye jamii kwa kuzua taharuki kupitia matukio ya utekaji yanayoripotiwa, wao na familia zao hawapo nchini, hivyo nchi ikiingia kwenye vurugu wao watakuwa salama.
“Kulizuka taharuki kubwa sana baada ya kupotea kwa huyu Padri, kama kawaida ya wapinzani hususani hawa wanaoishi nje ya nchi, wakavihusisha vyombo vya dola na Serikali na tukio hilo, matokeo yake ukweli umejulikana, Padri hakutekwa, bali amekimbia madeni,” alisema Mosses Mgonza, mkazi wa Ilala, Dar es Salaam.
Mgonza alisema, baada ya tukio hilo alikutana na ujumbe kwenye moja ya makundi ya mitandao ya kijamii ikiwataka Wakatoliki kutoshiriki uchaguzi unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025 kutokana na kile walichodai kutekwa kwa Padri huyo.
Hata hivyo alisema, aliamua kujipa muda kusubiri taarifa rasmi yya Jeshi la Polisi kabla ya kuamini yale yanayozungumzwa, kwani alianza kuwa na mashaka na baadhi ya matukio yanayotokea nchini.
“Kuna watu waliamini taarifa zilizokuwa zinasambazwa mitandaoni, wakapandwa na hasira, kumbe zilikuwa propaganda za wanaharakati, na hapo ndo unagundua sio kila tunachosoma mitandaoni kina ukweli, mengine yanatengenezwa ili kutugombanisha, ni vema sasa watanzania tukawa makini na tuviamini vyombo vyetu vya ulinzi na Usalama,” alisema.
Kwa upande wake Mwajuma Mwipi, mkazi wa Mbagala alisema, anaamini hakuna Serikali ambayo inaweza kuteka na kuua watu wake kwani Rais na viongozi wengine wameapa kuwatumikia wananchi, hivyo aliomba jamii kutoa ushirikiano ili kubaini chanzo cha matukio yanayotokea nchini ambayo mengine yanaonekana wazi yamechangiwa na ugomvi binafsi wa watu.
“Hili tukio la Padri limenifungua macho na akili, nimegundua kumbe huenda kuna matukio tunaambiwa yamefanywa na Serikali wakati sio kweli, jambo la kushukuru ni kwamba, Padri amepatikana akiwa hai, angepoteza maisha Habari ingekuwa nyingine,” alisema.
Mwajuma aliongeza, kupatikana kwa Padri huyo na sababu zilizotolewa na Jeshi la Polisi, zimewafunga mdomo waliokuwa wanatumia tukio hilo kuleta uchochezi, kwani walitaka kuwaaminisha watanzania kwamba, ametekwa kwasababu za kisiasa, jambo ambalo halina ukweli wowote.