REA yamshukuru Rais Samia

0

📌 Muitiko wa wananchi kutumia nishati safi ya kupikia waongezeka maradufu

📌 Mamia wajitokeza kupata elimu katika banda la REA

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umesema wananchi wameitikia kwa wingi wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu katika matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa Julai 12, 2025 na Afisa Upimaji Mwandamizi kutoka REA, Hussein Shamdas alipozungumza na vyombo vya habari kutoa tathmini ya ushiriki wa wakala katika maonesho hayo.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Kinara wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwani mamia ya wananchi waliotembelea banda la REA wameonyesha utayari wao katika kutumia nishati hiyo wakiwemo wazee, vijana hadi wanafunzi wa shule za msingi,” alisema Shamdas.

Alibainisha kuwa zaidi ya majiko banifu 100, majiko yanayotumia mionzi ya sumakuumeme (induction cooker) 450, pressure cooker 25 na majiko yanayotumia tungamotaka (biogas) 10 yaliuzwa katika kipindi cha maonesho hadi kufikia leo hii.

Alisema, miongoni mwa majukumu ya REA ni kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kote nchini na kwamba jukumu hilo ni endelevu na lengo ni kwamba, hadi kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi, wawe wanatumia nisnati safi ya kupikia kama ilivyoelekezwa kwenye Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Alifafanua kuwa katika utekelezaji wa jukumu hilo, REA itaendelea kushiriki katika Maonesho mbalimbali kote nchini yakiwemo Sabasaba, Nanenane, Wiki ya utumishi wa Umma sambamba na uhamasishaji kupitia mikutano ya hadhara, vyombo mbalimbali vya habari na kutoa elimu kwenye maeneo ya mikusanyiko.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi waliotembelea Banda la REA walimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kampeni hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia sambamba na kupongeza jitihada na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na REA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here