MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy pamoja na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Mzee Nyamka, wamesaini Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding – MoU) ya Utekelezaji wa Programu ya Ujenzi wa Miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye magereza 129 Tanzania Bara.
Katika utekelezaji wa Makubaliano hayo, REA italiwezesha Jeshi la Magereza katika Ujenzi wa Mifumo 126 ya Gesi Vunde (Biogas), Usimikaji wa Mifumo ya 56 ya Gesi ya Kimiminika (LPG), Uboreshaji wa Mfumo wa Gesi Asili katika Gereza Lilungu – Mtwara, Ununuzi wa tani 1,147 za mkaa mbadala (Rafiki Briquettes) na majiko 412, pamoja na Ununuzi wa Mashine 61 za kutengeneza Mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya mazao (Charcoal Briquettes).
Aidha, REA na Magereza zitashirikiana pia katika Usimikaji wa Mfumo wa Matumizi ya Gesi Asili katika Kaya 93 eneo la Gereza Keko, Kaya 548 katika Eneo la Ukonga Complex na majiko nane (ya Biashara eneo la Ukonga pamoja na utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi 280 wa Jeshi la Magereza kuhusu uendeshaji wa miradi ya nishati safi.
Itakumbukwa kuwa, Novemba 1, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo kwa Taasisi zote za Umma ambazo zinatumia nishati isiyo safi wakati wa kupika chakula cha watu wasiopungua 100, kuacha matumizi ya nishati chafu kwa ajili ya utunzaji wa mazingira pamoja na afya za watu.
Awali, katika hotuba yake, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Kizito Jaka, alisema Jeshi la Magereza lina jumla ya Magereza 129 katika mikoa yote Tanzania Bara ambayo yanahifadhi wastani wa wafungwa na mahabusu 32,000 kwa siku.
Aliongeza kuwa, vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia chakula cha wafungwa na mahabusu ni kuni kwa asilimia 98, mkaa mbadala kwa asilimia 0.9 na gesi asilia ni kwa asilimia 1.1, ambapo mahitaji ya kuni kwa ajili ya kuandaa chakula cha wafungwa na mahabusu magerezani ni mita za ujazo 69,017.5 kwa mwaka.