Nicolás Maduro
Na Benjamin Thompson
JANUARI 3, 2026, dunia iliamka na taarifa nzito iliyotikisa siasa za kimataifa. Vyombo vya habari vya Marekani, vikiongozwa na Fox News, viliripoti kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump akithibitisha kuwa jeshi la nchi hiyo limefanya mashambulizi ya kijeshi nchini Venezuela na kwamba Rais Nicolás Maduro “amekamatwa” na kuondolewa nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Taarifa hiyo, iliyotolewa na Trump mwenyewe, iligeuza kile kilichokuwa mgogoro wa kisiasa na kiuchumi kuwa tukio la kijeshi la wazi, na kuifanya Venezuela kuwa uwanja halisi wa makabiliano ya nguvu kati ya dola kubwa na taifa linalodai kulinda uhuru wake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mashambulizi yalifanyika alfajiri, yakihusisha mashambulizi ya anga na operesheni za haraka za kijeshi.
Ripoti za mitandaoni zilionyesha milipuko karibu na miundombinu ya usafiri wa anga na maeneo nyeti ya kijeshi, huku serikali ya Venezuela ikinyamaza kwa muda kabla ya kutangaza hali ya tahadhari ya kitaifa.
Ingawa bado kuna sintofahamu nyingi kuhusu hali halisi ya Maduro na uhalali wa madai ya Trump, kilicho wazi ni kwamba mgogoro wa muda mrefu umefikia hatua ya hatari.
Tukio hili halijatokea ghafla
Kwa miaka kadhaa, Trump amekuwa akisisitiza hadharani kwamba mafuta ya Venezuela ni “mali halali” ya Marekani kwa msingi kwamba kampuni za Marekani ndizo zilifanya tafiti za awali na kugundua akiba kubwa ya mafuta katika ardhi ya nchi hiyo.
Kwa mtazamo wa Trump, kusitishwa kwa mikataba hiyo na serikali ya Venezuela kulikuwa ni uonevu wa kiuchumi dhidi ya makampuni ya Marekani, na hoja hiyo imekuwa msingi wa shinikizo la kisiasa, vikwazo vya kiuchumi na sasa hatua za kijeshi.
Rais Nicolás Maduro, kwa upande wake, amekuwa akikanusha vikali madai hayo, akisisitiza kwamba Venezuela ni taifa huru lenye mamlaka kamili juu ya rasilimali zake. Mara kadhaa alinukuliwa akisema kuwa nchi yake iko huru kuuza mafuta yake kwa nchi yoyote duniani bila kuomba ruhusa ya Washington.
Kauli hizi ndizo zilizoifanya Serikali yake ionekane kama kikwazo kikubwa kwa maslahi ya Marekani katika sekta ya nishati ya Kimataifa.
Swali linalojitokeza sasa ni uhalali kwa hatua hii katika zama hizi tulizonazo? Kisheria, chini ya misingi ya sheria ya kimataifa, taifa lina haki kamili ya kusimamia na kumiliki rasilimali zake za asili. Mikataba ya kibiashara inaweza kurekebishwa au kusitishwa endapo itaonekana kukiuka maslahi ya taifa husika, ingawa suala la fidia kwa makampuni ya Marekani hubakia kuwa jambo la majadiliano ya kisheria zaidi.
Hivyo, hatua ya kijeshi ya moja kwa moja, inaibua maswali mazito kuhusu uvunjaji wa uhuru wa nchi na kanuni za Umoja wa Mataifa.
Historia inaonyesha kuwa hili si jambo jipya kwa Venezuela
Mtangulizi wa Maduro, Hayati Hugo Chavez, aliwahi kukumbana na misukosuko mikubwa kama hiyo alipodhamiria kurejesha udhibiti wa mafuta mikononi mwa serikali.
Chávez alikabiliana na mashinikizo makali ya Marekani, akiwemo jaribio la mapinduzi mwaka 2002, lililodaiwa kuungwa mkono na maslahi ya nje, hususan kutoka Marekani. Ingawa alirejea madarakani kwa nguvu ya wananchi na jeshi, alitawala chini ya kivuli cha uhasama wa kudumu na Washington hadi kifo chake mwaka 2013.
Katika zama za Maduro, mvutano huo ulizidi kuwa mkali zaidi. Maduro siyo mtu wa mchezo. Marekani iliweka vikwazo vizito vya kiuchumi, hasa katika sekta ya mafuta, kwa lengo la kukausha mapato ya serikali ya Caracas. Vikwazo hivyo viliifanya nchi hiyo ishindwe kuuza mafuta yake kwa uhuru katika masoko mengi ya kimataifa.
Serikali ya Venezuela ilieleza wazi kwamba lengo la vikwazo hivyo lilikuwa ni kumlazimisha Maduro atii masharti ya Marekani, ikiwemo kuruhusu kurejea kwa makampuni ya Marekani kuchimba na kuuza mafuta, kwa masharti yanayopendelewa na Washington.
Katika hatua zilizozua taharuki zaidi, Venezuela ilidai kuwa Marekani ilipeleka manowari na doria za kijeshi baharini ili kuzuia meli zilizokuwa zikielekea kununua mafuta ya nchi hiyo.
Ingawa Marekani ilijitetea kwa kusema ilikuwa inatekeleza vikwazo vya kimataifa, kwa macho ya wengi katika Amerika ya Kusini, hilo lilionekana kama kizuizi cha kijeshi cha wazi dhidi ya taifa huru.
Ukaribu wa Maduro na Urusi umechangia kwa kiasi kikubwa kile kinachoendelea leo. Ushirikiano wa kijeshi, kiusalama na kiuchumi kati ya Caracas na Moscow uliifanya Marekani kuona Venezuela kama tishio la kimkakati katika eneo lake la ushawishi.
Urusi ilijitokeza kama mshirika mbadala katika biashara ya mafuta na silaha, jambo lililoongeza hofu ya Marekani kwamba rasilimali za Venezuela zingetumika kuimarisha kambi pinzani katika siasa za dunia.
Hatua ya kijeshi ya Marekani, kama inavyoripotiwa sasa, inaweza kuwa kilele cha mkakati wa muda mrefu wa shinikizo. Ikiwa madai ya kukamatwa kwa Maduro yatathibitishwa, itakuwa ni mojawapo ya matukio adimu sana ambapo kiongozi wa taifa anatangazwa kuondolewa kwa nguvu na nchi ya nje katika karne hii, jambo litakalobadilisha kabisa mizani ya siasa za kimataifa.
Kwa nchi za Afrika, simulizi ya Venezuela ni onyo kali. Bara letu limejaa mifano ya nchi zilizoingiliwa kisiasa kwa kisingizio cha demokrasia, haki za binadamu au uwekezaji, ilhali lengo halisi likiwa ni rasilimali.
Pale viongozi wanapokataa masharti ya kibeberu, hufuatiwa na vikwazo, propaganda, migawanyiko ya ndani na wakati mwingine mapinduzi ya wazi au ya kificho.
Funzo kubwa ni kwamba uhuru wa kisiasa hauwezi kudumu bila uhuru wa kiuchumi. Nchi za Afrika zinapaswa kujifunza kujadiliana kwa umoja, kujenga taasisi imara na mikataba yenye kulinda maslahi ya wananchi wao.
Kitendo cha kukubali kuwa vibaraka wa nchi tajiri ni hatari inayoweza kuwa na watu wanaogeuza baraka za rasilimali kuwa laana ya migogoro na umaskini wa kudumu.
Venezuela pia inatukumbusha umuhimu wa mshikamano wa ndani ya nchi kama Waafrika. Migawanyiko ya kisiasa ilirahisisha shinikizo la nje kupata mianya. Afrika, yenye historia ya migawanyiko ya kikabila na kisiasa, inapaswa kutambua kuwa udhaifu wa ndani ni mpenyo wa kuingiliwa watu wabaya kutoka nje ya nchi.
Kwa lugha nyingine, mgogoro wa Marekani na Venezuela ni somo hai la namna rasilimali zinavyoweza kuwa sababu ya vita, siasa na mapinduzi.
Ni simulizi ya nguvu dhidi ya uhuru, maslahi dhidi ya haki, na shinikizo dhidi ya msimamo. Kwa Afrika, ujumbe ni mmoja: tusikubali kupandikizwa vibaraka ili rasilimali zetu ziibiwe, kwa maana historia inaonyesha kwamba tusipokubali, hatua kali hufuata. Lakini pia historia inatufundisha kuwa bila kusimama imara, uhuru wa kweli hubaki kuwa ndoto.