RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema nchi imepiga hatua kubwa kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano 15, hivyo kuongeza imani kwa Serikali.
Rais Dkt. Samia amesema hayo wakati wa kuhitimisha Shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bungeni Dodoma Juni 27, 2025.
Alisema, alipoingia madarakani aliahidi kudumisha Tunu za Taifa ikiwemo Mungano na hatua hiyo inaendeleza umoja wa Watanzania wenye ushirikiano licha ya tofauti za dini, mila, desturi, itikadi za siasa na michezo.
“Katika hotuba ya kufungua Bunge nilisistiza umuhimu wa Viongozi wa pande mbili za Muungano kukutana na kuzungumzia ustawi wa Muungano wetu, nafurahi kuwataarifu kwamba yale maagizo yangu yametekelezwa kwa ufanisi mkubwa chini ya Makamu wa Rais akisaidiwa na Waziri Mkuu kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar ni Makamu wa Pili wa Rais,” alisema.
Pamoja na hayo, Rais Dkt. Samia aliwaasa Watanzania kuendelea kushikamana na kuendeleza amani na sifa njema kwa nchi ya Tanzania.