Rais Samia kuzindua zoezi la ujazaji maji bwawa la Nyerere

0

Na Beatrice Sanga – MAELEZO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la kushuhudia ufungaji wa lango la handaki mchepuko (diversion tunnel) ili kuruhusu maji kuanza kujaa katika bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere litakalofanyika Disemba 22, 2022.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika eneo la mradi wa umeme wa Mto Rufiji Waziri wa Nishati January Makamba alisema, mradi huo una hatua kubwa mbili ambazo zina hadhi ya kushuhudiwa na kusherehekewa, ambapo hatua ya kwanza ni kufunga lango la njia ya mchepusho wa maji na ya pili ni kuwasha mitambo ya kufua umeme

“Kwa ujumla hadi leo mradi huu umefikia hatua ya asilimia 78, ni hatua kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na katika hatua za mradi, mradi huu una maisha na kuna alama ambazo tunafikia siku zote na hatua

“Tumemaliza kujenga tuta, barabara, tumemaliza kujenga nyumba za wafanyakazi kwahiyo kuna mafanikio katika kipindi chote, sasa tumefikia kwenye mafanikio makubwa tangu tuanze ujenzi wa mradi huu na yenyewe ni kujaza maji kwenye bwawa, kazi ya kujenga handaki la kuchepusha maji ilifanyika miaka mitatu iliyopita na handaki hilo lina urefu wa Mita 700 na ujenzi uligharimu Shilingi Bilioni 235,” alisema Makamba.

Makamba alisema, kutokana na umuhimu wa hatua hiyo ya mradi ulipofikia, hatua hii ya kuanza kujaza maji kwenye bwawa itazinduliwa na na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Rais atabonyeza kitufe ambacho kitashusha geti la kuziba handaki lilikuwa linachepusha maji na rasmi maji yataanza kujaa kwenye bwawa.

Aliongeza kuwa, shughuli hiyo itahudhuriwa na watu takribani 2000 wakiwamo viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na viongozi wengine kama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri, Makatibu Wakuu, wakuu wa Mikoa na Wilaya zinazozunguka Bonde la mto Rufiji, viongozi wa Dini, Viongozi wa Chama na wananchi.

Vile vile, kutakuwa na ugeni kutoka Misri ambako ndiko wanatoka wakandarasi wanaojenga mradi huo, wakiwemo mawaziri, viongozi wa serikali pamoja na vyombo vya Habari, wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo.

Akizungumzia faida za mradi huo Makamba alisema, ndani ya Serikali mradi huu ni mpana zaidi na utasaidia pia katika masuala ya Kilimo chini ya mto Rufiji, Uvuvi, Kuondoa mafuriko, Upatikanaji wa huduma za maji wa uhakika kwa Jiji la Dar es Salaam, Utalii, miundombinu na usafirishaji pamoja na kupata umeme wa uhakika.

Naye Mkurugenzi wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Maharage Chande alisema, inakadiriwa kwamba misimu miwili ya mvua itaweza kufanya bwawa Hilo la Julius Nyerere kujaa maji hivyo zinatazamiwa mvua za masika Machi 2023 na 2024 kuweza kujaza Bwawa hilo.

Mradi wa kufua umeme kwa njia ya maji wa Julias Nyerere ambao unakadiriwa kuzalisha megawati 2115, ulianza kujengwa mwaka 2019 na unatarajiwa kukamilika June 2024 na umegharimu kiasi cha Shilingi Trilioni 6.5 ukiwa umebakisha asilimia 22 mpaka kukamilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here