Rais Samia aweka jiwe la msingi kongani ya viwanda

0

Na Albert Kawogo, Pwani

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa kongani ya viwanda katika eneo la Kwala, Kibaha mkoani Pwani, ambalo linatarajiwa kuwa na zaidi ya viwanda 200.

Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 31, 2025, ambapo tayari viwanda saba vimeanza kufanya kazi na vingine vitano viko katika hatua za ujenzi.

Kongani hiyo ya viwanda katika eneo la Kwala, pamoja na Bandari Kavu ya Kwala, inatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa Taifa na wananchI kupitia ajira, biashara, shughuli za ujenzi, na usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi.

Dkt. Samia alisema, mradi huo mkubwa wa kimkakati utasaidia kuzalisha ajira za moja kwa moja 50000 na kuongeza kiwango cha uchumi kwa wakazi wa eneo hilo

“Kongani hii (Kwala) itakuwa na uwezo wa kutoa ajira za moja kwa moja 50,000 na zisizo za moja kwa moja kama 150,000,” alisema Rais Samia.

Awali, akiongea wakati akiweka jiwe la Msingi kwenye eneo litakapojengwa kongani ya Viwanda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo ameeleza kuwa, kujengwa kwa Kongani ya Viwanda na uzinduzi wa Bandari Kavu Kwala mkoani Pwani, kutatengeneza ajira 300,000 ikiwemo ajira za moja kwa moja 50,000, suala ambalo litawezesha kuzalisha ajira kwa vijana wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.

Dkt. Jafo alisema, ujenzi wa kongani ya Kwala utafanikisha ujenzi wa viwanda 200 katika eneo hilo kwa uwekezaji wa Dola Bilioni 3, suala ambalo litawezesha mauzo ya mwaka ya Dola Bilioni 6, 2 zikiwa mauzo ya nje na Dola Bilioni 4 zikiwa mauzo ya bidhaa mbalimbali ndani ya Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania (TPA) Wakili Plasduce Mbossa alimweleza Rais jinsi TPA itakavyoweza kurahisisha utoaji wa mizigo kutoka bandari ya Kwala kwenda sehemu nyingine tofauti za ndani na nje ya nchi utakavyoweza kuunganishwa kwa njia ya reli

Mbossa pia alisema, bandari ya Kwala ina eneo la hekta 502 ambalo ni mara tano ya ukubwa wa bandari ya Dar es Salaam huku eneo hilo likiwa limezungushiwa ukuta wa hekta 60.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here