Rais Samia awafuta machozi ya kuni akinamama nchini

0

📌 Atoa Ruzuku ya Shilingi Bilioni 9.4 kwenye Majiko Banifu

📌 Kaya 200,000 kunufaika

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza mradi wa Shilingi 9,400,799,626.7 wa kusambaza majiko yaliyoboreshwa maarufu kama majiko banifu 200,000 kwa bei ya ruzuku ya asilimia 80 hadi 85 kote nchini.

Hayo yamesemwa Agosti 4, 2025 na mwakilishi wa REA Mkoani Morogoro, Mhandisi Cecilia Msangi wakati akimtambulisha Mtoa huduma aliyeshinda zabuni ya kusambaza majiko hayo Mkoani humo, kampuni ya Burn Manufacturing Tanzania Ltd katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

“Wakala unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia miradi mbalimbali ikiwemo huu wa kusambaza majiko banifu ambao rasmi leo hii tupo hapa kuutambulisha kwa wananchi wa Morogoro,” alisema Mha. Msangi.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kampeni hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo alisema kwa jitihada zake binafsi hatua mbalimbali zimechukuliwa hususan za kuwanusuru akina mama kutokana na madhara ya moshi wa kuni sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Alisema, Rais Samia alitoa maelekezo mahususi ya kuhakikisha wananchi wanawezeshwa ili kuachana na matumizi ya kuni na mkaa kupikia ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umeelekeza ifikapo Mwaka 2034; 80% ya wananchi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumza juu ya utekelezaji wa mradi kwa Mkoa wa Morogoro, Mha. Msangi alisema jumla ya majiko banifu 8,366 yatatolewa kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 14,694 kwa kila jiko.

“Kwa bei ya kawaida kabla ruzuku jiko hilo lilikuwa likiuzwa Shilingi 73,468.36 na sasa baada ya kupokea kwa ruzuku ya 80% jiko hilo litauzwa kwa Shilingi 14,694 tu,” alibainisha Mhandisi Msangi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mussa Mussa alipongeza jitihada za REA na alisema kuwa manufaa yatakayopatikana kutokana na mradi huo ni makubwa kuliko hata inavyotarajiwa.

“Haya majiko namna yalivyosanifiwa yanatumia mkaa kidogo na pia yanatunza joto kwa muda mrefu, hivyo inakwenda kumpunguzia mwananchi gharama za mkaa na kumuokolea muda,” alisisitiza Katibu Tawala, Musa.

Aidha, mwakilishi wa Mtoa huduma Kampuni ya Burn Mkoani humo, John Mtui alisema kampuni yao imeshinda zabuni ya kusambaza majiko banifu 39,286 katika Mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Kagera na Tabora ambayo ni sawa na Shilingi 2,309,022,392.77.

“Hapa Morogoro tutasambaza jumla ya majiko 8,366 katika Wilaya za Gairo, Kilombero, Kilosa, Malinyi, Morogoro Vijijini, Ulanga na Mvomero ambapo kila wilaya itapata majiko 1,196,” alisema Mtui.

REA inatekeleza miradi mbalimbali nchini kwa kuwezesha na kuelimisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama kwa afya zao na mazingira kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here