Rais Samia asisitiza maslahi ya Taifa kwenye mikataba

0

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaendelea kuzingatia maslahi ya nchi kwenye Mikataba mbalimbali ambayo nchi inakusudia kuingia.

Alisema, Kikatiba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo yenye dhamana ya upekuzi na Tathmini ya Mikataba inayoingiwa na Serikali na Taasisi zake.

Dkt. Samia ameyasema hayo Februari 3, 2025, wakati alipokuwa Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria nchini 2025 yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali Jijini, Dodoma.

Aidha, Dkt. Samia amewataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kuzingatia Weledi wakati wa kufanya Upekuzi na Tathmini ya Mikataba mbalimbali ambayo Serikali inayokusudia kuingia.

“Katika kuhakikisha masilahi ya nchi yetu yanaendelea kuzingatiwa kwenye Mikataba itakayoingiwa ni lazima Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wawe na uwezo na ubobevu kwenye masharti ya Kimikataba yanayogusa sekta za kiuchumi na uwezo wa kusimamia mikataba hiyo,” alisema Dkt. Samia.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alisema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea Kufanya upekuzi na tathmini kwenye Mikataba mbalimbali ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2024 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikuwa imepekua Mikataba 1,799 na Hati za Makubaliano 352.

“Kati ya mwezi Julai hadi Disemba, 2024 jumla ya Mikataba ya Kitaifa, Kikanda na 10 Kimataifa 1,799 na Hati za Makubaliano (Memoranda of Understanding) 352 zilifanyiwa upekuzi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika hatua nyingine Johari alisema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuwahimiza Mawakili wa Serikali na Wanasheria wote walioko katika utumishi wa umma kujiendeleza na kushiriki mafunzo ya fani mbalimbali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here