Na Jumbe Abdallah
RAIS Samia Suluhu Hassan ameziagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufuatilia miradi ya maendeleo iliyobainika kuwa na dosari.
Rais Samia alitoa agizo wakati akihutubia kwenye hafla ya maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 na kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere iliyofanyika katika Uwanja wa Kaitaba, Mkoani Kagera.
Alisema, vitendo vya rushwa vinajirudia kwa kuwa viongozi katika maeneo mbalimbali hawafuatilii maendeleo ya miradi ya wananchi hadi Mwenge wa Uhuru unapopita na kubaini dosari hizo katika miradi hiyo.
“Kila mwaka tunapokea taarifa za kilele cha mbio au taarifa ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali) tunasomewa na kutajiwa maeneo ambayo Mwenge umekataa kuizindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi iliyopo katika baadhi ya halmashauri,”
“Pia ile ambayo utekelezaji wake umekiuka kanuni za ujenzi au miradi kutumia fedha nyingi za umma ikiwa chini ya kiwango kinachokubalika.” alisema Rais Samia.
Aliendelea kusema: “Hali hii inajirudia kila mwaka… Tunaposomewa taarifa za Mwenge wa Uhuru kila mwaka kuna miradi inayojirudia ni vitendo vya rushwa, uvujaji wa fedha na mambo mengine. Kila CAG anapokabidhi ripoti yake vitendo vinajirudia,”
Ili kukabiliana na hali hiyo, Rais Samia amewataka viongozi na watendaji wahakikishe wanasimamia matumizi sahihi ya fedha zinazoelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Hapa kuna swali kubwa la kujiuliza wakati miradi hii inajengwa, viongozi tupo na tunaona, lakini hakuna kinachozungumzwa wala kusema hadi Mwenge wa Uhuru upite, huu sio mtindo mzuri,”
“Inasikitisha kuna watu wasiojali wala kuhurumia wananchi, wenye vitendo viovu ya kuwapa miradi wakandarasi wasiokuwa uwezo, waliotawaliwa na vitendo vya rushwa na wizi. Wengine wakiwa wazembe wanaosababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo.
“Yanatokea haya viongozi tukiwa bado tupo, katika ngazi zetu tofauti, kuanzia Taifa, mikoa, wilaya hadi halmashauri. Tunaona lakini tunasubiri vijana wakimbiza mwenge waje kusema miradi mibovu na haiendani na fedha zilizotumika,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema, licha ya kazi nzuri inayofanywa na TAKUKURU na ZAECA, lakini bado zinahitaji kusaidiwa na vyombo vingine ili kuendelea kufanya kazi ya kudhibiti vitendo vya rushwa.
“Tungekuwa wote tunazungumza kauli moja vitendo hivi vingeonekana mapema na taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa. Tunachokifanya ni kupambana na baada ya Mwenge kuibua kero katika kuzuia hatujafanya vizuri, ongezeni jitihada katika upande huu,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wasiojali na kuhurumia wananchi kwa kuwapa miradi wakandarasi wasio na uwezo na kusababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa Aprili 2, 2022 ambapo miradi ya maendeleo 1,293 iliyogharimu Shilingi Bilioni 650.8 ilizinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi katika maeneo mbalimbali nchini.