Na Edmund Salaho, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amebainisha mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya Maliasili na Utalii kwa kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Rais Samia alibainisha hayo wakati akihutubia na kuhitimisha Shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Juni 27,2025, ambapo alisema Serikali imechukua hatua mahususi kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kukua zaidi na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
Kutokana na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali, kuna ongezeko la idadi ya watalii wa Kimataifa kwa asilimia 132.1% kutoka watalii 922,692 kwa mwaka 2021 hadi watalii 2,141,895 mwaka 2024.
Vile vile, Rais Dkt. Samia amebainisha ongezeko kubwa la watalii wa ndani kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi watalii Millioni 3,218,552 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 307.9%
Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa maboresho yaliyofanywa kwenye sekta ya utalii yamechochea ongezeko la ajira kwa vijana wa kitanzania kupitia sekta ya utalii ambapo idadi ya wakala za Biashara za utalii zimeongezeka kutoka 2,885 mwaka 2020 hadi kufikia 3,735 mwaka 2025.
“Idadi ya waongoza watalii imeongezeka kutoka waongoza watalii 5,076 mwaka 2020 hadi kufikia idadi ya waongoza watalii 7,662 mwaka 2025”
Pia, mapato yatokanayo na utalii yamepanda kutoka Dola za Kimarekani Milioni 700 mwaka 2020 hadi kufikia Bilioni 3.9 mwaka 2024.