Na Albert Kawogo, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.. Samia Suluhu Hassan kesho Alhamisi, Julai 17, 2025 anatarajiwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya maendeleo kuelekea 2050.
Uzinduzi huo ambao unatarajia kufanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention, jijini Dodoma, ni hatua ya mwisho ya mchakato wa maandalizi ya dira hiyo, uliodumu kwa miaka miwili.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, amesema hayo leo Julai 16, 2025 wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma.
“Dira hii ni muhimu kwani itakwenda kutoa mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 25 ijayo,” alisema Dkt. Msemwa na kuongeza, maandalizi ya Dira hiyo yamehusisha wananchi kutoka makundi mbalimbali.
“Tulipokea maoni kutoka kwa Watanzania takribani Mlioni 1.174 kupitia njia mbalimbali, na zaidi ya watu 20,000 walihudhuria makongamano ya Kitaifa yaliyolenga kuibua maono ya pamoja kuhusu mustakabali wa Taifa letu,” alisema Dkt. Msemwa.
Hata hivyo, amefafanua kuwa Tume ilifanya utafiti wa kina kwa nchi zilizofanikiwa kufikia uchumi wa kati ili kujifunza mbinu bora zinazoweza kutumika katika kufanikisha malengo ya Tanzania, hususan kujenga uchumi wa kati kwa njia endelevu.
Rasimu ya Dira hiyo ilirudishwa kwa wananchi kwa ajili ya uhakiki wa mwisho, kuhakikisha maoni yao yamezingatiwa.
Baadaye, nyaraka hiyo ilijadiliwa na makundi ya kijamii, sekta binafsi, na wataalamu, ili kuhakikisha inawakilisha matakwa ya Taifa kwa mapana.
Aidha, Dkt. Msemwa ameeleza kuwa utekelezaji rasmi wa Dira ya 2050 utaanza Julai 2026, mara baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2025.
Alisema, Tume ya Taifa ya Mipango inaendelea kusimamia kwa karibu maandalizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu ili kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo shirikishi, jumuishi na endelevu kwa wananchi wote.