Pelekeni tabasamu kwa wananchi kiutendaji – Prof. Shemdoe

0

OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe amewataka watumishi na viongozi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa upendo, amani na mshikamano ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa ubora na kuachiwa tabasamu kupitia huduma zinazotekelezwa na Serikali.

Akizungumza mara baada ya kupokelewa na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI katika Makao Makuu ya Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma, Prof. Shemdoe amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuwaachia Watanzania tabasamu ifikapo mwaka 2030, na kusisitiza kuwa TAMISEMI ina jukumu la moja kwa moja katika kutimiza azma hiyo.

Amesema watumishi wanapotekeleza majukumu yao katika ngazi ya mikoa, wilaya, halmashauri, kata, vijiji, mitaa na vitongoji wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazoendana na mahitaji yao na kwamba tabasamu linalotarajiwa kwa wananchi linapaswa kuanzia kwa watumishi wenyewe kupitia utendaji uliokamilika na wa kuheshimu utu.

Aidha, Prof. Shemdoe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuongoza wizara hiyo, pamoja na wananchi wa Lushoto waliompa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia kama Mbunge wa Jimbo hilo.

Kwa upande wa Naibu Waziri anayeshughulikia afya, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Reuben Kwagilwa amesema wizara itaendelea kuongeza ushirikiano na ufanisi ili kuhakikisha sekta hiyo inatoa huduma bora zinazochochea maendeleo na kuongeza tabasamu kwa wananchi.

Naye Naibu Waziri wa anayeshughulikia masuala ya Afya TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa weledi na ushirikiano ili kuboresha huduma za Afya hususan katika ngazi ya Afyamsingi ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri wote wateule kutekeleza kwa kasi ahadi 100 za Serikali ya Awamu ya Sita ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uhakika na kwa wakati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here