Na Iddy Mkwama
WAKALA wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PETROLEUM BULK PROCUREMENT AGENCY – PBPA) imeweka wazi mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mkuu wa PBPA Erasto Simon alitaja mafanikio hayo Agosti 7, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa habari uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina (TR).
Alisema, kwa kipindi cha miaka minne, idadi ya kampuni zinazoshiriki kwenye mchakato wa uagizaji wa mafuta zimeongezeka kutoka 33 mwaka 2021 hadi kufikia kampuni 73 mwaka 2025, ambalo ni ongezeko la asilimia 121.
Aidha, alisema wamefanikiwa kusajili jumla ya wazabuni 24 katika Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS) kwa kupindi cha miaka minne kutoka mwaka 2021 hadi 2025.
“Kiwango cha uagizaji wa mafuta kupitia mfumo wa BPS kimeongezeka kutoka wastani wa Tani 5,805, 193 mwaka 2021 hadi Tani 6,365,985 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 9.6 na hadi Disemba 2025,,” alisema Simon.
Aliongeza: “Jumla ya Tani 7, 090,165 zitakuwa zimeagizwa ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 11.4 ikiliganishwa na kupindi hiki kwa mwaka uliopita.”
Mafanikio mengine ambayo ameyataja ni kuongezeka kwa zabuni za uletaji wa mafuta nchini, ambapo mwaka 2021 zilikuwa 109, lakini hivisasa hadi kufikia Disemba zinatarajia kufika 118.
“Mikataba ya zabuni za uagizaji wa mafuta nchini imeongezeka kutoka wastani wa mikataba 109 mwaka 2021 hadi kufikia wastani wa mikataba 118 ifikapo Disemba 2025. Jumla ya mikataba 589 kwa miaka minne imetekelezwa kwa ufanisi,” alisema.
Pia, PBPA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupanga ratiba za meli zinazoleta shehena ya mafuta, ambapo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wameongeza ufanisi wa matumizi ya bandari zilizopo nchini na kupunguza gharama za meli kusubiri (demurrage).
“Hatua hii imesaidia kuokoa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 11.5 sawa na Bilioni 29.95 fedha za Kitanzania kwa mwaka, fedha ambazo zilikuwa zinatumika, hivyo hatua hii imesaidia kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini, ambazo awali zilikuwa zinatumika kulipia gharama husika,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisema, eneo jingine ambalo wamefanikiwa, ni kutunza taarifa za mafuta yanayoingia nchini kupitia Mfumo wa BPS, na kuanzia Julai 2024, PBPA imeanza kusimamia na kutunza taarifa za meli zote zilizo nje ya Mfumo wa BPS zinazoshusha mafuta nchini, hivyo kuwa na taarifa sahihi za mafuta yote yanayoingia nchini.
“Uwekezaji katika maghala ya kuhifadhia mafuta nchini umeongezeka kutoka maghala 22 mwaka 2021 hadi 24 mwaka 2025, huku uwezo wa kuhifadhi ukiongezeka kutoka lita Milioni 1,288. 101 hadi lita Milioni 1,721,327. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 34,” alisema na kuongeza kuwa, ongezeko hilo limechochewa zaidi na upanuzi mkubwa wa maghala katika jiji la Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusu hali ya upatikanaji wa mafuta nchini, Simon alisema imeendelea kuwa ya uhakika katika kipindi cha miaka minne iliyopita kutokana na uongozi madhubuti wa Serikali ya Awamu ya Sita.
“Serikali imeiwezesha PBPA kukabiliana na changamoto mbalimbali za kidunia kama UVIKO -19 na vita baina ya Urusi na Ukrain na vita baina ya Iran na Israel. Katika kipindi chote, nchi imekuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji wakati wote pamoja na kuhudumia nchi jirani,” alisema.
Aidha, alisema wakala huo umefanikiwa kufunga mfumo wa kusimamia upokeaji wa mafuta nchini (flowmeters na SADA), hatua ambayo imesaidia kudhibiti udanganyifu katika kiasi cha mafuta yanayopokelewa kwenye maghala ya kuhifadhia nishati hiyo.
“Mifumo hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza upotevu wa mafuta, kwa kufunga mifumo hiyo, Serikali ya Awamu ya Sita imeokoa kiasi Shilingi Bilioni 56.4 kila mwaka na hivyo kwa miaka minne, imeokoa Shilingi Bilioni 225.6 zilizokuwa zinapotea kutokana na upotevu wa mafuta,” alisema.
Vile vile alisema, kwa kipindi cha miaka minne watumishi wapya 68 wa kada mbalimbali wameajiriwa kwa ajili ya kuendelea kutekeleza majukumu ya kuratibu uagizaji wa mafuta nchini pamoja na usimamizi wa Mfumo wa BPS.
“Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja (PBPA) umeendelea kuboresha usimamizi wa mfumo wa BPS ili kuendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini wakati wote na kwa bei stahiki zinazoendana na mwenendo wa mabadiliko ya bei katika soko la dunia,” alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema, maboresho ya usimamizi huo umezivutia nchi za jirani ambazo zinategemea bandari za Tanzania, huku akiahidi kwamba, PBPA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya mafuta vikiwemo vyombo vya habari katika kuimarisha mfumo wa BPS kwa maslahi mapana ya Taifa.
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) ni moja ya taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Nishati, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali, Sura ya 245.
Majukumu ya jumla ya Taasisi hii ni kusimamia mfumo wa Uagizaji wa Pamoja wa mafuta nchini na kuhakikisha mafuta yanaletwa kwa njia yenye ufanisi (efficient procurement) na kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya nchi wakati wote.