OMO, Lissu wamevigharimu vyama vyao Angola

0

Mwandishi Wetu

MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman ‘OMO’, mwenzake wa Chadema, Tundu Lissu na wafuasi wao, hivi karibuni walizuiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Luanda, nchini Angola.

Walikataliwa wasiingie nchini humo kuhudhuria Mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia (PAD), OMO kwenye msafara wake, aliambatana na Dorothy Semu (Waziri Kivuli wa chama hicho wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa} na Dkt. Nasra Nassor Omary.

Walijaribu kufanya jitihada tofauti ili kuingia nchini humo lakini waligonga mwamba, hivyo walilazimika kurudi nchini na kupokewa na wenzao wa vyama vyao waliowaacha nyumbani.

Tundu Lissu katika mtandao wake wa X (zamani twitter), alilalamika kuwa mamlaka za Uhamiaji za Angola zimewazuia na kukataa kuwaruhusu kuingia nchini humo.

Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria kama ilivyo kwa mwenzake, OMO wa ACT Wazalendo, anadai kuwa si wao pekee bali pia ujumbe wa viongozi wengine takribani 20 wamezuiwa.

Anasema pia kuna waliotokea Kenya, Sudan, Rais wa zamani wa Botswana, Waziri mkuu wa zamani wa Lesotho, Namibia na Eswatini.

Pia, kulikuwa ujumbe wa Namibia, Lesotho, Ujerumani, Marekani, Uganda, DR Kongo na Msumbiji.

”Kama Angola wapo SADC sisi hatuhitaji visa, huu ni udhalilishaji kwa raia wa Mataifa ndugu ya Afrika unayofanywa na Mamlaka za Angola,” analalama Lissu.

Anaenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa waliyofanya (kuwazuia wao), hayakubaliki. “Yanapaswa kulaaniwa na kwa maneno makali kabisa”.

Anabainisha kuwa, udugu na urafiki upo baina ya Tanzania na Angola toka kipindi kile cha harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma, anawalalamikia wanaoshangaa kuzuiwa kwake.

Miongoni mwa wanaoshangaa kuzuiwa kwao pamoja na Makamu Mwenyekiti CCM Taifa, Steven Wassira na Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya chama hicho chini ya Khamis Mbeto Khamis.

Wassira Machi 14, 2025, akiwa Tunduma anasema amesoma sehemu viongozi wanaenda Angola wamenyang’anywa pasipoti, huko ni Angola sio Tanzania na anasema kuwa pengine walikuwa na jambo lao, wanalitilia shaka.

Mjumbe wa NEC Zanzibar na Katibu Mwenezi na Mafunzo wa kama hiyo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis nae anashangaa vipi mwanasheria nguri kama OMO asijue itifaki za safari za viongozi na kujikuta akikwama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Luanda Angola.

OMO anasema, kuwashangaa wao ni kuipaka matope serikali na hazungumzii alipokwamishwa hadi akajikuta anashindwa kuingia katika nchi hiyo ambayo ina historia ya udugu na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Makamu huyo wa kwanza wa Rais ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), anayetarajia kuwania Urais Oktoba mwaka huu 2025, badala ya kueleza kiini pengine kilichomfanya azuiwe kulingana na hao waliomkatalia asiingie kwao, anawalalamikia wanaohoji ufahamu wake katika masuala ya diplomasia.

Anamlalamikia Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Mbeto Khamis Mbeto na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Steven Wasira kwa kauli zao kuwa pengine OMO hakufuata utaratibu au hajui utaratibu wa kusafiri nje.

OMO anadai kuwa, wanachama hao waandamizi wenye nafasi nyeti katika chama kinachotawala pande mbili za Muungano, wameipaka matope Serikali kufuatia kitendo hicho.

Anasema viongozi hao wamefanya upotoshaji, Makamu wa Rais (yaani yeye OMO), anasafiri kwenda nje, Serikali inamuachia, haichukui hatua za kufuata taratibu za Kidiplomasia na protoko” analalama Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo.

Anasema, anaongea ili watanzania wajue tuna viongozi gani katika Serikali ya CCM, lakini kilicho bayana ni kuwa wananchi wajue watakuwa na mgombea wa aina gani wa Urais kutoka ACT Wazalendo.

Kauli ya OMO kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais (yaani yeye OMO), anasafiri kwenda nje, Serikali inamuachia, haichukui hatua za kufuata taratibu za kidiplomasia na protoko ni kauli tata.

Ni kauli ambayo katika akili ya kawaida kabisa unajiuliza hivi alichukua hatua gani Serikali kutambua safari yake na tena ndio ifuate na sio OMO afuate? Inafikirisha.

Nani anasafiri? OMO au Serikali? Kama yeye angekamilisha taratibu za kidiplomasia na protoko inavyotaka, alioambatana nao angewaacha wapi?

Lissu nae ingekuwaje? Au ndio nae angejibananisha na itifaki ya OMO na kitendo kilichofanywa na wanasiasa hao kimevigharimu vyama vyao.

Leo hatujui nguvu za kiuchumi za ACT Wazalendo hadi kumgharamia OMO na wanachama hao wengine wawili safari yao, lakini Chadema wanatembeza bakuri la ‘Tone tone’ kuchangia chama.

Kama pesa za michango ya wanachama ndivyo zinavyotumika kulipana posho, kusafiri bila kufuata utaratibu na kuishia viwanja vya ndege ni wazi kuwa upinzani una safari ndefu.

OMO na Lissu wanapaswa kuwaomba radhi wanachama wao na pia kutambua kuwa elimu haina mwisho hivyo kuwa mwanasheria pekee hakutoshi kukufanya kujua kila kitu, ndio maana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anawaita VETA wenye digrii wakaongeze ujuzi.

Elimu ya Sayansi ya siasa na masuala ya uongozi yanahitaji kupewa nafasi na kila mwenye kusudio la kuwatumikia wananchi kinyume cha hivyo tutaendelea kushuhudia vituko vya kisiasa vya ACT Wazalendo na Chadema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here