MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema katika dhima nne (4R’s) za Rais Samia Suluhu Hassan, Ofisi ya Msajili wa Hazina imechukua ‘R’ mbili za ‘Reforms na Rebulding,’ ambazo wataendelea kuzisimamia.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Mchechu alisema, mabadiliko ya utendaji wa Taasisi ni safari ndefu, ndio maana wanajitahidi kuweka msingi bora wa kufikia malengo yanayokusudiwa.
Mchechu kupitia mkutano huo alisema, yapo matukio mawili makubwa ambayo watayatumia kwa ajili ya kujipima na kujiandaa kufikia malengo hayo ambayo yatafanyika hivi karibuni; tukio la kwanza ni Siku ya Gawio kwa Serikali, pili Mkutano wa wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (CEO’s Forum)
Alisema, wakati Rais Samia akifungua kikao chao cha kwanza mwaka jana, jijini Arusha, aliwaagiza kuanza kuangalia fursa za uwekezaji wa Mashirika hayo ya Serikali nje ya nchi.
“Tukio la kwanza ambalo litakuwa linafanyika kila mwaka litakuwa ni kuhusu gawio kwa sababu hilo tukio la gawio kama lilivyofanyika tarehe 11 mwezi wa 6 mwaka huu. Hii ni kwa taasisi zote kwenda kurejesha magawio yao kwa Mheshimiwa Rais au kutimiza wajibu wao wa kisheria.”
“Litakuwa inafanyika kila mwaka. Tukio la pili ni kama hili la kikao tunachokwenda kufanya Arusha, nalo ni tukio la kila mwaka. Haya ni matukio yetu mawili makubwa ambayo tutakuwa tunayapa umuhimu wake,” alisema Mchechu.
Aidha, alisema wanaamini kwamba, matukio hayo mawili yatawasaidia kuwajibika kwa jamii, ambapo kauli mbiu ya mkutano ujao itakuwa ni “Mikakati ya Mashirika na Taasisi za Umma kuwekeza Nje ya Tanzania”.
Akitolea mfano Mashirika kama ATCL, alisema ingawa linatambulika kwa huduma zake kupatikana nje ya nchi, lakini ofisi zake zinapaswa ziende nje na kugusa jamii ya huko kwa ufanisi na ushindani mkubwa.
“Mfano wa pili ni Kampuni kama TRC na TAZARA, ni kampuni ambazo ili zifanye vizuri katika huduma zake ni lazima ziguse usafirishaji unaovuka mipaka ya nchi yetu na kwa kufanya hivyo, tutaweza kupata maslahi ya kile tulichokiwekeza huko.”
“Kwa hiyo tunapozungumza ‘investment beyonds Tanzania,’ ni kuangalia nini tunaenda kufanya nje. Lakini zipo nyingine zinazoweza kwenda kufanya uwekezaji kabisa nje ya nchi, tunatamani mabenki yetu makubwa yawe na uwekezaji mkubwa nje ya mipaka yetu, wawe na matawi yao nje ya Tanzania.
Alisema, kuna Benki ya CRDB ambayo imefika Burundi na sasa wanaenda DRC, hivyo CRDB au NMB kwa uwekezaji wao nje ya nchi, wameshakua wakubwa ndani ya nchi yetu.
“Sasa maana yake ni nini? NMB leo hata wakiwa na Tawi Zambia, kukiwa na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika mikoa ya Mtwara au Lindi, hawatoumiza kichwa namna ya kufanya miamala ya kibiashara katika nchi za Zambia au Malawi, kwa sababu tayari ana benki ambayo ina matawi ndani ya nchi na nje,” alisema.
Mchechu alisema, ndio maana Wakenya, wananufaika na uwepo wa matawi ya benki zao za KCB na Equity ambazo zipo Tanzania, hivyo ni rahisi kwa Mkenya kufanya biashara kwa ufanisi nchini, na kwamba Tanzania nayo inapaswa kuwa mahiri, lakini ianze katika ngazi hizo.
“Kikao hiki kina umuhimu mkubwa, ikiwemo kujua maagizo na maelekezo ya Serikali kupitia viongozi wakuu ya wapi wanataka tuelekee na kwa kasi gani, ikiwa ni pamoja na Maafisa watendaji wakuu na Wenyeviti wa bodi kubadilishana mawazo na mbinu mbalimbali za uendeshaji biashara,” alisisitiza Mchechu.