MSAJILI wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema, Shilingi Bilioni 900 zimekusanywa kutoka kwenye taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache zipatazo 200.
Akizungumza katika kikao na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, leo Juni 2, 2025, alisema wana shauku ya kukusanya Shilingi Trilioni 1 na iwapo Ofisi hiyo itafanikiwa kukusanya kiwango hicho, itakuwa ni ongezeko la asilimia 30.4 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita ambapo walikusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 767.
“Hadi kufikia sasa (Juni 2, 2025) Ofisi ya Msajili wa Hazina imekusanya karibia Shilingi Bilioni 900 kama mapato yasiyo ya kodi na matamanio yetu ni kukusanya Shilingi Trilioni 1 katika mwaka wa fedha wa 2024/25.” alisema Mchechu.
Aidha, Mchechu alisema ili kuhakikisha Ofisi hiyo inafikia adhima hiyo ya kukusanya Shilingi Trilioni 1, alizitaka taasisi ambazo bado hazijawasilisha gawio zifanye hivyo ndani ya wiki hii.
“Taasisi zote ambazo bado hazijawasilisha gawio kwa Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, zinapaswa kufanya hivyo ndani ya wiki hii ili ifikapo siku ya Gawio, Juni 10 mwaka huu, asiwepo wa kudaiwa,” alisema.
Alisema, ukuaji wa mapato yasiyo ya kodi umetokana na kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika Mashirika ya umma na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.
“Ofisi imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Mpango na Bajeti (PlanRep) na Mifumo ya ERMS na e-Watumishi pamoja na kufanya maboresho ya Mfumo wa MUSE ambao unawezesha kupata taarifa halisi za matumizi katika Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za Umma,” alisema Mchechu.
Alisema, maboresho hayo sasa yamefanya mifumo kubadilishana taarifa ipasavyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuona mifumo inasomana.
Katika hatua nyingine, Mchechu alisema mageuzi na mabadiliko ya kifikra katika kuendesha taasisi na mashirika ya umma ni nguzo muhimu ili kuleta ufanisi, uwajibikaji na maendeleo endelevu nchini.
“Kwa hiyo, katika taasisi zote lazima kuwe na mabadiliko chanya kuhakikisha mali tulizokabidhiwa zinakuwa na matokeo chanya.