SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limekamilisha rasmi ujenzi wa nyumba 68 mpya katika eneo la Iyumbu, Jijini Dodoma, na sasa nyumba hizo zimeingia sokoni.
Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi mkubwa wa makazi, ambapo jumla ya nyumba 300 zimejengwa na kukamilika.
Picha zilizopigwa leo mchana Septemba 19, 2025 zinaonyesha wazi mandhari ya kuvutia ya nyumba hizo, zikithibitisha kwa vitendo dhamira ya NHC ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na ya kisasa.
Nyumba hizi zimejengwa katika eneo lenye mazingira ya kimkakati, karibu kabisa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), na kuifanya Iyumbu kuwa kitovu bora cha makazi kutokana na utulivu wake, ukaribu na huduma muhimu pamoja na miundombinu iliyoimarika.
Wananchi wote wanakaribishwa kununua nyumba hizi, ambazo zinajivunia ubora wa ujenzi, mpangilio wa kisasa na bei nafuu zinazomuwezesha kila Mtanzania kumiliki makazi bora.
Kwa hatua hii, NHC inaendelea kusimama imara katika kutimiza ndoto ya Watanzania ya kuwa na makazi bora, ikidhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya nyumba.